Hapana shaka Youthe Rostand alifanya vizuri akiwa na African Lyon katika msimu juzi kabla ya msimu jana kuvaa jezi ya wana Jangwani.
Timu ya Wananchi!, timu yenye mashabiki wengi hapa Tanzania, kwa kifupi ni timu yenye presha kubwa ndani na nje ya uwanja.
Ilikuwa hatua kubwa kwake kutoka African Lyon na kwenda Yanga.
Moja ya timu ya ndoto ya wachezaji wengi, wengi huamini ngozi zao zikivaa jezi ya Yanga au Simba zitanawiri kuliko kuvaa jezi ya timu nyingine hapa Tanzania.
Inawezekana ni kweli ! , ndiyo maana wengi huwa wanakimbilia Kariakoo , wenye malengo hufanikiwa kutoka hapo na kwenda sehemu nyingine.
Ila kuna kitu kimoja tu ambacho wengi huwa wanasahau kipindi ambacho wachezaji wengi wanapofika Kariakoo, nacho ni kuwa jezi za timu za Kariakoo ni nzito!.
Hazina wepesi hata kidogo kama jezi za timu zingine hapa Tanzania, mashabiki wengi wa Kariakoo kwao wao wanaamini kila msimu lazima wachukue ligi kuu. Kila msimu lazima amfunge mwenzake kwenye mechi kati ya Simba na Yanga.
Hapa ndipo presha inapoanzia, mchezaji hutakiwa kufahamu kuwa kila anapoingia uwanjani anatakiwa aipe timu yake alama tatu ambazo zitaisaidia timu kubeba ubingwa.
Kwa Yanga na Simba hakuna kitu kinachoitwa kupoteza mechi, kwao wao kuna kitu kinachoitwa kushinda mechi pekee.
Ndiyo maana Youthe Rostand alifanya vizuri na African Lyon na akafanya vibaya na Yanga kwa sababu African Lyon hawana mahitaji sawa na Yanga.
Yanga wanamahitaji mengi na makubwa kuzidi African Lyon,ndiyo maana hata ukifanya kosa African Lyon halitoonekana kama ambavyo utafanya kosa ukiwa umevaa jezi ya Yanga.
Baada ya Youthe Rostand , Yanga walilihitaji mchezaji ambaye anauwezo wa kuendana na presha ya timu.
Aendane na kelele za mashabiki. Ahakikishe kuwa anauwezo wa kuipambania timu kwa presha ya aina yoyote ndiyo maana walimleta Kindoki.
Waliamini ni golikipa wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa wa kucheza katika presha ya aina yoyote ile!.
Lakini mapema tu ameanza kuonesha kuwa inawezekana jezi ya Yanga ikawa nzito kwake. Tunaweza kusema labda bado mapema, tumpe muda!.
Lakini wakati tunaendelea kumpa muda tunatakiwa kumtazama mara mbili mbili Beno Kakolanya.
Golikipa Mtanzania, nahisi neno “Mtanzania” ndilo lilomnyima haki ya kuibeba Yanga.
Tangu kipindi cha Youthe Rostand alionekana ndiye mtu sahihi wa kusimama katika ile milingoti mitatu.
Lakini hakupewa nafasi labda kwa sababu ya kasumba yetu ya kuamini wageni hata kama hawana uwezo mkubwa kutuzidi sisi.
Neno “mgeni” huchukuliwa kwa tafasri tofauti, mchezaji ambaye anakiwango kikubwa kuzidi mchezaji wa ndani.
Inawezekana ni kweli kwa sababu kuna baadhi ya wachezaji wenye viwango vikubwa kuzidi wachezaji wa ndani.
Lakini ukweli unabaki pale pale kuna wachezaji wa nje hawana viwango vya kuwazidi wachezaji wa ndani. Mfano halisi ni kwa Youthe Rostand na Kindoki, hawana uwezo wa kumzidi Beno Kakolanya na hofu yangu ni moja tu, huenda neno “U-Tanzania” linapambana na neno “Mgeni” ndiyo maana Beno Kakolanya anakuwa mhanga kwenye hii vita.