SHABIKI mwandamizi wa Ajax Amsterdam, Mart Van Hoidonk mwaka 1996, alitoka uwanjani mpira ukiwa mapumziko na kuamua kurudi nyumbani. Rafiki yake aliyekuwa nyumbani alimshangaa Hoidonk aliyemuaga anakwenda uwanjani kutazama mpira, akirudi kabla mpira wenyewe kumalizika.
Hoidonk kwa sauti yake ya chini alimwambia rafikiye kuwa asimshangae kurudi kabla ya mpira kumalizika na kuongeza kuwa kwa kiingilio alichokitoa alipaswa kutazama mchezo kwa dakika 45, kama angetaka kuumalizia mchezo huo angepaswa kulipa tena kiingilio cha nyongeza na kama hana kiingilio hicho ni bora arudi nyumbani sio kudhulumu jasho la wachezaji wa Ajax kitu. Ajax walikuwa moto.
Ajax Amsterdam, langoni alikuwa Edwin Van De Sar, kulia Michael Risiger, kushoto Marco Van Broncost, ndani Philipe Cocu na Ronald Koemam. Defensive Midfielder Edgar Davis, kulia Frank De Boer, kiungo wa mbele Claulence Seedof, striker Nwako Kanu baadae anaingia Patrick Kluivert, inside ten Dennis Berghamp, wingi ya kushoto ina Ronald De Boer.
Kila nikimtazama mke wangu Nasma wakati huu najiona Hoidonk ndani yangu. Najiona kuna dhuluma nimeifanya kwenye malipo ya mahali. Kwa jinsi alivyo Nasma sikupaswa kulipa nilichokilipa. Nilipaswa kulipa kingi kingi zaidi. Mke wangu mzuri, mnyenyekevu, msikivu. Dunia ishapungukiwa wanawake wa aina hii.
Nasma ana sauti nzuri kama Bi Asia, ana umbo zuri kama Bi Mariam, ana mwendo mzuri kama Bi Khadija. Ana tabia njema kama mama yangu Bi Arapha. Mengine ni siri yangu. Nasma utaniua. Now najihisi kama ng’ombe aliyepata mfanyakazi mpya anayemjali kwenye matunzo yake na kumpa malisho yanayostahili. Kiufupi niko peponi. Siku zangu nne kwenye maisha ya ndoa ni kama nina siku 400. Allah jaalia upendo huu udumu hadi siku ya Qiama.
Mkeyenge sijakosea kwa Nasma. Raha iliyoje ni jina la Nasma kuwa na maana ya uzuri. Nikisema na kuwaambia mke wangu mzuri mnielewe kuwa namaanisha na simsifii kutokea hewani. Nasisitiza jamani mke wangu mzuri.
Dunia ina wanawake wachache aina ya Nasma. Hawa ni wanawake wanaojua kuishi na mtu katika mazingira ya namna yoyote ile. Watakaliopinga hili, wengi wao hawajaoa. Waliooa wenzangu wanajua naelezea kitu gani hapa. Msiooa kuweni wapole tu tusikilizeni kaka zenu tuliooa.
Kwa hizi raha ninazopata sasa kuna haja ya kuifuata njia Hoidonk. Hakuna namna tena. Njia yenyewe ni kuongeza mahali nyingine. Nikiendeleza ubishi nitakuwa namdhulumu mzee yule mkarimu aliyepiga goti lake chini na kunikabidhi bintiye kwa moyo mkunjufu.
Uungwana ni jambo zuri, haswa ukipendezewa na huduma. Nimeipenda huduma ndio maana nimeona nilichokilipa hakiendani na huduma ninayopata. Yote tisa kumi Nasma anampenda Allah (S.W) na Mtume wetu Muhammad (S.A).
Narudia tena ni wanawake wachache wanaoweza kumjua mungu na kufuata mafundisho yake. Nasma ni mmoja wa kwenye hili. Anapenda sana mafundisho mema, nitakuwa na kesi ya kujibu siku ya mwisho kama Nasma atabadilika kwenye mikono yangu na kuzifuata njia za shetani. Namuomba Allah aniongoze kwenye hili.
Ilani yangu. Atakayemuona Wema Isaac Sepetu kokote pale anifikishie ujumbe wangu kuwa Mkeyenge na mke wake wanamsalimia.