Hapana shaka mwaka huu ulianza na mshindo mkuu, mshindo ambao ulitokea katika jiji la Manchester na kusambaa duniani.
Kila sehemu duniani kote watu wengi walikamatwa hisia zao kutokana na usajili wa Alexis Sanchez.
Hiki ni kitu cha kawaida sana kwa klabu kubwa kama Manchester United, klabu ambayo inajua kucheza na akili za watu ili wanufaike na biashara yao ya mpira
Kwao wao mpira ni biashara kuanzia nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja, ndiyo maana unaweza ukawaona hawachukui makombe makubwa kama kombe la ligi kuu ya England lakini kwenye suala la utajiri ndiyo klabu tajiri duniani.
Inajua namna ya kufanya biashara ndani pamoja na nje ya uwanja.
Pesa zao kwa Paul Pogba zilirudi kabla hata ya Paul Pogba kukanyaga nyasi za Old Traford .
Walitengeneza mazingira ya kuuza jezi kabla zake kwa manufaa ya klabu , na mazingira haya yalianza kutengenezwa kwa kulifanya jambo la Pogba kuwa kubwa , kila mtu aliongelee watu watamani kuwa na jezi namba 6.
Pesa ikaingia kwenye akaunti zao, maisha yakaendelea mpaka yakafika siku ambayo Alexis Sanchez alitakiwa kwenda Manchester United kutoka Arsenal.
Hakuna hela waliyotoa kumnunua Alexis Sanchez zaidi ya kubadilishana wachezaji, lakini kwao wao halikuwa jambo dogo.
Haikuwafanya wao wasiwe na uchungu kisa hawajatoa hela ya kumnunua. Wakatengeneza mazingira mazuri, mazingira ambayo yatamvutia kila mmoja na awe na shauku na Alexis Sanchez.
Mazingira haya yalimfanya Alexis Sanchez azaliwe upya na kuonekana kuwa mkubwa zaidi ya yoyote kwenye ligi ya England.
Lilikuwa jambo la kushangaza kipindi Alexis Sanchez anaenda Manchester United kukutana na shabiki wa Manchester United akimpandisha Alexis Sanchez kwenye daraja la kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo hii ni kwa sababu ya mazingira yaliyotengenezwa na kitengo cha biashara ya Manchester United.
Mazingira ambayo yaliongeza matamanio kwa mashabiki, wakajivunia kuwa na Alexis Sanchez na kumuona moja ya nyota mkubwa kwenye sayari hii.
Jezi namba saba (7) aliyokabidhiwa ndiyo ikawa msumari wa mwisho kwenye mioyo ya mashabiki wa Manchester United , matamanio ya kununua jezi yake ikawa kubwa.
Mauzo ya jezi yake yalienda kwa kasi kubwa, Manchester United ikawa imeshafanya biashara kubwa nje ya uwanja, macho na masikio ya wengi wakawa wanasubiri namna ambavyo Alexis Sanchez atafanya vizuri ndani ya uwanja.
Matamanio yalikuwa makubwa sana, kiasi kwamba kila shabiki alitamani kila mpira uwe unamfikia Alexis Sanchez ili afanye mambo makubwa.
Mambo ambayo yalikuwa yanachagizwa kutokana na usajili wake kuwa na nguvu pia na jezi yake namba saba ambayo iliwahi kuvaliwa na watu wazito ambao walifanya mambo makubwa katika timu ya Manchester United.
Miamba kama Brayn Robson “Captain Marvel”, Eric Cantona, David Beckham na Cristiano Ronaldo waliwahi kufanya vitu vitakatifu wakiwa ndani ya joho lenye namba 7.
Tangu 2009 , Cristiano Ronaldo alipovua Joho hilo, kila aliyekuwa anajaribu kulivaa lilikuwa linampwaya.
Wengi walisubiri ni nani atakayeweza kulivaa joho hili aonekane limemtosha ipasavyo, Alexis Sanchez alibeba matumaini mengi kwenye hili.
Matumaini ambayo mpaka sasa yanaishi kwa sababu haimanishi ameshashindwa kufanya vizuri na jezi hii, lakini matumaini ya mashabiki yamepungua.
Mechi 9 akiwa na goli moja pamoja na pasi tatu za mwisho za magoli ni jambo ambalo linaonesha mwanzo usio wa kishindo kwake.
Wakati mashabiki wanatamani kishindo kikubwa kutoka kwa Alexis Sanchez, Jose Mourinho anatamani kuona kishindo kikubwa kutoka kwenye timu yake.
Jose Mourinho anataka timu yote kwa ujumla ifanye vizuri, hata kama mchezaji mmoja asipofunga cha muhimu kwake ni kuona mchango wa mchezaji huo umesaidia kushinda mechi husika.
Ndipo hapo matamanio ya kocha na mashabiki yanapotofautiana. Kocha matamanio yake yanaongozwa na msukumo uliopo ndani yake, wakati mashabiki matamino yao huongozwa na namna ambavyo wanataniwa na wapinzani wao.