Sambaza....

Where Am I ? Ni moja ya kitabu bora kabisa cha mwanafilosofia Daniel Dennett alichokiandika mwaka 1978.

Kitabu ambacho alikitumia kuelezea umuhimu wa akili ya mwanadamu.

Akili ambayo MUNGU aliiweka kichwani mwa mwanadamu kwa makusudi makubwa sana.

Moja ya kusudi kubwa ni kumfanya mwanadamu aweze kutafasri kile anachokiona na kutafasri kitu kabla ya mdomo wake haujakitoa nje.

Na ndipo hapo Daniel Dennett alijikita, hakuuonea huruma wino wa kalamu yake kuelezea umuhimu wa kutafasri kitu unachokipokea na unachokitoa katika mazingira yako ya kila siku.

Mazingira ambayo yanatukutanisha na vitu vingi ambavyo hugeuka changamoto na vingine hugeuka kuwa njia ya mafanikio .

Changamoto au mafanikio hukaribishwa na mwanadamu mwenyewe.

Hii ni kutokana na jinsi ambavyo ubongo wake unatafasri vipi vitu vinavyoingia ili kumpa nafasi tena ya kutafasri vitu anavyovitoa nje, hapo ndipo mafanikio au changamoto ya mwanadamu huanzia.

Wengi wetu hupata changamoto, changamoto ambazo huyumbisha mpaka dira yetu ya maisha na kusahau kabisa sehemu ambayo tulikuwa tunaitamani awali kwenda.

Ndoto zote hupotea pale umakini na nidhamu vinapokosekana kwa sababu macho ya akili huwa yanapata upofu.

Upofu ambao husababisha tusijue ipi njia sahihi ambayo tunatakiwa kupitia.

Ndiyo wakati ambao mwanadamu hutumia msumeno kumenyea viazi akiamini ni kitu sahihi na anaweza kukifanya kwa ufasaha.

Hii yote ni kwa sababu tunakosa washauri wazuri ambao ushauri wao hutumika kama mwongozo wa njia bora ambazo tunatakiwa kupitia.

Washauri ambao ni wachache sana kwenye nyaja mbalimbali hasa hasa kwenye michezo.

Ndiyo maana vipaji vingi hufa mapema kabla ya umri wa kustaafu. Inauma unapoona mtu mwenye kipaji anastaafu akiwa kwenye umri mdogo.

Na hii ni kwa sababu hakuna watu wazuri wa kuwashauri ili waweze kuingiza kitu ambacho wanauwezo wa kukitafsri vyema vichwani mwao ili hata wanapokitoa kwa matendo kisiwaathiri wao kama wao.

Daniel Dennett kwenye kitabu chake cha “Where Am I?” anatabainisha kuwa endapo mtu akiwa na washauri wabaya hata vitu ambavyo ubongo hutafasri na kuvitoa nje kwa njia ya mdomo au matendo huwa ni vibaya.

Image result for mohamed ibrahim mo images

Kuzungukwa na watu wabaya kunakufanya umtengeneze wewe mbaya. Wewe ambaye hauna maono , wewe ambaye hauna njaa ya mafanikio , wewe ambaye hauna nidhamu.

Nidhamu mbovu ambayo inaweza kukuharibia mwelekeo wako wa maisha na kukuingiza katika shimo ambalo litazika kila kitu ambacho ulichonacho.

Ni mapema sana kusema Mohamed Ibrahim amepoteza kila kitu alikuwa nacho, ila ni vyema kumpa tahadhari kuwa anaweza kupoteza kila kitu alichonacho.

Anahitaji kusaidiwa msaada mkubwa wa mawazo ya kumjenga na kumtoa kwenye njia aliyokuwa anataka kupitia.

Njia ambayo ilikuwa inataka kuangamiza ndoto zake , anatakiwa akumbuke matamanio yake ya awali aliyokuwa nayo wakati ameamua kuufanya mpira kama sehemu yake ya kujiingizia kipato.

Akumbuke safari ndefu aliyo nayo, safari ambayo inahitaji jitihada zake ili afike, hatakiwi kuruhusu kitu chochote kibaya kikarudisha nyuma jitihada zake.

Kuna wakati utafika , wakati ambao utakuwa mgumu kwake yeye kuweza kurudisha siku nyuma. Nyakati ambazo zitakuwa na majira magumu kwake kuyameza.

Ndizo nyakati ambazo huwa tunashuhudia ugumu wa mate ya mlevi kufika chini ya ardhi zaidi ya kifuani kwake.

Ndiyo maana siogopi na sichoki kumkumbusha kuwa Samaki wa futari hatiwi ndimu.

Atumie muda huu ambao kisima chake kina maji mengi kuchota na kujengea nyuma yake imara ya muda mrefu, kuna siku kisima chake kitaisha maji na akakosa hata maji ya kupikia chai, na ukizingatia maji ya dafu hayapikiwi ndimu ndipo hapo ataona thamani ya kutumia maneno ya nyakati zilizopita, “ningejua, ningetumia kichwa changu kuiongoza miguu yangu”


Sambaza....