Simba sc, imetinga mzunguuko wa kwanza wa michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kuiondosha Gendermarie ya Djibouti kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0.
Huo unaweza kuwa ni mwanzo mzuri kwa klabu hiyo ya Tanzania wakishiriki kwa mara ya kwanza baada ya takribani misimu minne kupita, na sasa watakutana na klabu ya Al Masri ya nchini Misri.
Al Masri sio klabu ya kubeza sana, ni moja ya vilabu vikubwa nchini Misri ikishiriki ligi kuu ya nchini humo na kwa sasa wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, klabu hii ya Al Masri maarufu kama Green Eagles ilianzishwa Machi 18, 1920, uwanja wao wa nyumbani ni Port Said Stadium wenye uwezo wa kubeba watazamaji 17,000 na kocha wao wa sasa ni gwiji wa soka nchini humo Hossam Hassan.
Ubora wa ligi wanayoshiriki, na aina ya kocha waliyenae ni moja ya vitu vinavyonishawishi kusema klabu hiyo sio ya kubeza Hossam Hassan ana uzoefu mkubwa na mpira wa Afrika, alicheza kwa mafanikio makubwa kuanzia ngazi ya klabu na timu ya taifa ya Misri lakini pia anafahamu vema aina ya mpira wa Tanzania, na nikiiangazia ligi kuu ya nchini humo bila shaka ni moja ligi bora kabisa barani Afrika yenye ushindani mkubwa sana kwa kulinganisha na ligi yetu ambayo Simba sc wanashiriki ni wazi hii pia ni changamoto.
Labda niseme kuwa sina nia ya kuwatisha/ kuwaogopesha Simba sc la hasha ila ni kujaribu kuwakumbusha kuwa maandalizi na mikakati madhubuti inahitaji sana kuelekea katika mchezo huo, kwa kuzifahamu vema na kabla mbinu za wapinzani wao hawa na pia wachezaji wanaopaswa kupewa uangalizi maarumu.
Sina shaka sana na uwezo wa kikosi cha sasa cha Simba sc, kuanzia benchi lake la ufundi linaloongzwa na Mfaransa Pierre Lechantre kwa maana naye ni kocha mwenye uzoefu mkubwa lakini pia rekodi zikionesha aliwahi kufanya kazi katika nchi za Afrika ya Kaskazini hivyo ni wazi atakuwa anafahamu aina ya mpira wa timu zinazotoka ukanda huo.
Lakini kama hiyo haitoshi pia klabu ya Simba imekuwa na rekodi nzuri kwa kulinganisha na vilabu vingine nchini katika ushiriki wake kwenye michuano ya kimataifa, ikianzia mnamo mwaka 1974 ilipofka nusu fainali ya michuano ya vilabu bingwa barani Afrika, pia itakumbukwa mwaka 1993 iliwahi kufika fainali ya kombe la Caf ambalo sasa linaitwa kombe la shirikisho baada ya kubadili jina hilo, hii ni rekodi ambayo kwa Tanzania hakuna klabu iliyofikia, na ni wazi haikufika hapo kwa bahati nasibu ila ilikuwa na kikosi kipana kilichokuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa sana nawazungumzia Mohammed Mwameja, Deo Mkuki, George Masatu, Raphael Paul, Malota Soma, Edward Chumira, George Lucas hawa ni baadhi waliokuwa chini kocha mzawa Abdallah Kibadeni aliyesaidiwa na Etienne Eshente kutoka Ethiopia, Manzini wanderers, Feravialio De Maputo na Atretico club Aviacao ni baadhi vilabu vilivyochezea kichapo cha kikosi hicho.
Lakini kama hiyo haitoshi pia Simba sc, mnamo mwaka 2003, iliwahi kuwaondosha waliokuwa mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa barani Afrika hapa naizungumzia Zamalek ya Misri wanakotoka wapinzani wao wa sasa (Al Masri).
Pia Simba sc, imekuwa na rekodi nzuri inapocheza kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya timu kutoka Afrika ya Kaskazini, kitu kinachoniongezea imani kubwa kuwa Simba wanauwezo wa kuwaondosha Waarabu hao wa Misri
Rekodi za Simba sc kunako kombe la Caf/ Shirikisho tangu mwaka 1993
Raundi ya kwanza
Simba sc (Tanzania) vs Ferraviario (Msumbiji) 0-0 1-1 Simba wakafudhu kwa faida ya goli la ugenini
Raundi ya pili
Simba vs Manzini wanderers (Swaziland) 1-0 1-0 Simba wakapata ushindi wa jumla mabao 2-0
Robo fainali
Simba vs El Harrach (Algeria) 3-0 2-0 jumla 3-2
Nusu fainali
Simba vs As Aviacao (Angola) 3-1 0-0 jumla 3-1
Fainali
Stella Abidjan (Ivory coast) vs Simba 0-0 2-0 Stella wakatwaa ubingwa kwa ushindi wa mabao 2-0
Mwaka 1997
Raundi ya kwanza
Simba vs Afc Leopards (Kenya) 1-1 0-3 jumla 1-4
Mwaka 2007
Raundi ya awali
Textile de pungue (Msumbiji vs Simba 1-1 1-1 jumla 2-2 Simba ilitolewa kwa penati 3-1 hii ndio mechi ambayo iliondoka na maisha ya kiungo wa zamani wa vilabu vya Simba na Yanga, marehemu Said Mwamba “Kizota” na huu ulikuwa mchezo wa marejeano ulipigwa Februari 11, jijini Dar es salaam
Mwaka 2010 raundi ya kwanza
Lengthens FC (Zimbabwe) vs Simba 0-3 1-2 jumla 1-5
Raundi ya pili
Simba vs Haras El Hodood (Algeria) 2-1 1-5 jumla 3-6
Mwaka 2011
Baada ya Simba kuondolewa kunako michuano ya ligi mabingwa ikaangukia kwenye kombe la shirikisho kuwania kufudhu hatua ya makundi
Simba vs DC Motema Pembe (DRC) 1-0 0-2
Mwaka 2012
Simba vs Es Setif (Algeria) 2-0 1-3 jumla 3-3 Simba ikapita kwa faida ya bao la ugenini