Kwa taarifa tu ni kwamba baada ya pambano la Simba na Yanga mnamo Jumanne ya Julai 19, Mwaka 1977, mwaka uliofuatia wa 1978 Yanga na Simba hawakukutana mwaka huo.
Mwaka huo ligi ilianzia ngazi ya kanda, halafu washindi wa kila kanda walikuja Dar es salaam kwa fainali.
Timu 6 zilifuzu kushiriki fainali, ambazo zilikuwa Simba, Yanga, Pan, Navy ya Zanzibar (ambayo sasa ndiyo hii KMKM), Pamba ya Shinyanga na Coastal Union ya Tanga.
Yanga walianza kwa sare ya 0-0 na Navy, halafu wakafungwa 2-0 na Pamba ya Shinyanga.
Baada ya mechi hiyo, Yanga wakajitoa kwenye ligi wakilalamikia kuonewa na waamuzi.
Wakasema wakiendelea kucheza na kuonewa, mashabiki wao wanaweza kuleta vurugu. (Hapa inaonyesha ni kwa kiasi gani kuwa mashabiki wa Gongowazi ni watu wa vurugu na shari long time kitambo!)
Kwa hiyo walijitoa hata kabla ya kukutana na Simba.
Vilevile kabla ya hapo Uto walijitoa pia katika miaka ya 1965, 1966 na 1967. Ingawa hii ya mwaka 1967 walijitoa wote wawili yaani Simba na Yanga.
Mwaka 1970 kimsingi ligi haikumalizika kabisa kwani Yanga na Simba wote waligoma.
FAT iliruhusu timu za makampuni na mashirika kushiriki ligi.
Na hizo timu ndizo wachezaji wa Yanga na Simba walikuwa wanafanya kazi.
Kwa hiyo zilishiriki, wachezaji wakachezea timu za makazini kwao. Yanga na Simba wakapinga sana hilo.
FAT ikalazimisha, jamaa mapacha wa Kariakoo wakajitoa.
Lakini Uto ndiyo haswa wanaongoza kwa kujitoa mara nyingi zaidi.
Ligi ikashindwa kuendelea.
FAT wakaiteua Yanga ikashiriki klabu bingwa Afrika, kwa sababu ndiyo ilikuwa Mabingwa wa msimu uliopita, yaani mwaka 1969.
Wakati huo ligi inachezwa kwa mwaka wa kalenda.
Baada ya kuteuliwa, Yanga wakajitangaza mabingwa.
Kimsingi mwaka1970 Yanga hawakuwa Mabingwa uwanjani.
Ndiyo maana sisi wengine tunaamini Yanga ni Mabingwa mara 27, na siyo mara 28 kama mnavyodai nyinyi Uto, Mihogo FC, kwa sababu mwaka 1970 hamkushinda ubingwa.
Hii alinipenyezea mdogo wangu Zaka Zakazi baada ya kumuomba ufafanuzi kutaka kujua baada ya Mnyama kumchakaza Utopwenga mwaka 1977 mbona sioni rekodi yoyote ya mechi ya watani hawa wa jadi kwa mwaka huo wa 1978? Ndipo akanidadavulia hii. Ila mwaka 1979 pale “Shamba la Bibi” Uto mlichezea kichapo cha 3-1 mabao ya Nicodemus Njohole, Mohamed Bakari Tall na Abbas Dilunga huku bao la Uto likifungwa na Rashid Hanzuruni. Mechi hii matokeo yake nayakumbuka vizuri kwani siku hiyo tulikuwa tukisafiri kwa basi la Shirika la Reli, mabasi yao tukiyaita “Relwe” ( Railways) kutoka Mbeya kwenda Morogoro na tulipofika Ilula, Iringa abiria mmoja alimuuliza matokeo ya mechi hiyo mwenyeji wa pale Ilula wakati tunakula chakula hotelini na akamwambia kuwa Simba ameshinda kwa magoli 3-1.
Mwaka 1980 Uto pia walichezea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Mnyama. Mabao ya Abdallah Mwinyimkuu, Nicodemus Njohole na Thuweni Ally “Mpemba.”