Kocha mkuu wa klabu ya Azam Yousouf Dabo amekosa sifa ya kuwa kocha mkuu na uongozi wa klabu yake unafahamu hilo.
Dabo ambaye ni Msenegal Hana leseni ‘A’ ya CAF ambacho ni kigezo kikubwa cha kuwa kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu, badala yake anamiliki Leseni ‘B’ ya CAF ambayo aliipata muda mrefu.
Leseni ‘B’ ya CAF anayomiliki Dabo haimfanyi hata awe kocha msaidizi kwenye klabu ya Ligi Kuu, ili apate leseni ‘A’ ni lazima afanye “refresher course” kisha awe kwenye mazingira ya kufanya Leseni ‘A’.
Kwa kulijua hilo uongozi wa klabu ya Azam wakaamua kumuajiri kocha Bruno Ferry ambae ndio aliye jina lake ndiyo limepelekwa TFF kama kocha mkuu wa Azam FC.
Ajabu ni kwamba TFF wanamruhusu Dabo kuongoza timu kwenye mechi za Ngao ya Jamii pale Tanga ilihali wanajua kwamba hastahili hata kuwa kocha msaidizi.
Mambo ya msingi wanayafanya kiushikaji kitu ambacho kinaharibu hata hadhi ya Ligi kuu, lakini viongozi ambao hawawezi kusimamia kanuni walizotunga wenyewe ni watu wa kuogopa sana, kwakuwa maslahi binafsi yanakuwa mbele ya maslahi ya mpira.
Azam FC wanashiriki kombe la Shirikisho la CAF na Dabo huenda asiruhusiwe kukaa hata kwenye benchi kwa kukosa sifa, lakini kwenye Ligi namba 5 bora Afrika tunaogopana na kuleta ushkaji.
Said Kazumari