Ni miaka kumi sasa imepita tangu Azam alipotwaa kombe la ligi kuu Tanzania bara, kwa wakati huo ikitambulika kama Vodacom Premier League.
Katika miaka hii kumi iliyopita Simba na Yanga zimekua zikipokezana kubeba ubingwa wa ligi, Azam walitegemewa kuwa wapinzani wa kweli kwa Simba na Yanga lakini stori ilikua tofauti kwani hawakuwa na muendelezo wa kiwango kizuri kiasi cha kuwa mabingwa kama walivyofanya msimu wa 2013/14.
Licha ya Azam kuwa na kila hitaji la timu ya mpira wa kisasa lakini walishindwa kuitika wito na kuendana na kasi ya mapacha wa Kariakoo (Simba na Yanga) kiasi cha kushindwa kutoa upinzani mkubwa.
Naaaaaaam!! Azam wameitikia wito sasa, Azam wamejipata, katika miaka hii kumi iliyopita ya kujiuliza maswali mengi juu ya kupokea na kuitikia wito huu sasa wameitika, kwani wamefanya usajili mkubwa wa kukidhi mahitaji ya kocha na benchi lake la ufundi, maboresho makubwa ya utawala na benchi la ufundi ni dalili tosha kuwa Azam wameitika wito wa kwenda kupambania kikombe cha ligi msimu ujao unaotarajiwa kutimua vumbi mapema mwezi huu.
Mwingine atasema oooh Azam ndio zao hao tushwazoea kila siku kusajili lakini hakuna kitu! Mwingine atauliza kwani kusajili Azam ameanza leo mbona huko nyuma amesajili lakini matokeo kiduchu? Kivipi wameitikia wito angali ni mabadiriko ya kawaida ambayo yamezoeleka?
Nikutoea shaka ndugu msomaji, Kandanda.Co.Tz iko hapa kukujuza na kukuhabarisha juu ya itiko la wito la Azam kwa vilabu vya Simba na Yanga, nakusihi baki na Kandanda.Co.Tz kupata majibu yote ya maswali yako kama ifuatavyo;
● Usajili wa wachezaji wakubwa!
Msimu huu Azam haijasajili tu sababu wanatakiwa kusajili bali wamesajili wachezaji ambao ni wakubwa, Azam imesajili wachezaji ambao washakomaa tayari haihitaji tena kuwapa muda kuzoea mazingira. Kwamfano usajili wa kiungo Feisal salum “Feitoto” na MVP wa ligi kuu ya Tanzania bara msimu wa 2021/22 Yanick Bangala wote kutoka Yanga ni viashilia vya kuutaka ubingwa.
Wachezaji wakubwa huleta matokeo makubwa na Azam sasa wamechagua matokeo makubwa, lakini pia wamewabakisha wachezaji wao wote muhimu kwa kuwaongezea mikataba na kuifanya Azam kukamilika katika maeneo yote ya msingi na kubwa zaidi wamezingatia mahitaji ya benchi la ufundi kwa kusajili wachezaji pendekezwa.
● Mabadiliko ya Benchi la Ufundi!
Kila vita na mbinu zake, kila jeshi na kiongozi wake. Naam Azam wameitikia wito wa vita kubwa na wakubwa hivyo imewalazimu kufanya mabadiliko makubwa ya benchi la ufundi ili kuendana na kasi na ukubwa wa vita ya kuwania ubingwa wa ligi msimu ujao.
Ujio wa benchi jipya la ufundi utaleta tija kwa timu kwa kuibua morali na hali za wachezaji ukizingatia Azam wamejipangia mambo makubwa ya kuyafikia hivyo wamelipanua benchi lao la ufundi ili kuendana na ukubwa wa malengo ya klabu.
●Kambi na Maandalizi Mazuri
Azam waliweka kambi nchini Tunisia ili kujifua na kujiweka tayari kwa msimu mpya wa mashindano. Wakiwa huko Tunisia walicheza michezo kadhaa ya kirafiki dhidi ya timu zenye hadhi na za daraja la juu barani Afrika kama vile Esperanca de Tunis ya Tunisia, Al hilal Khartoum ya Sudan, na Us Monastrir ya Tunisia.
Wachezaji wakionekana wakiwa na uchu na morali ya ushindi ilionekana iko juu, hii inaonyesha wako kamili kuelekea msimu mpya wa mashindano. Azam wamerejea nchini juma lililopita ili kujiandaa kwa michezo ya Ngao ya jamii pale Mkwakwani Tanga ambamo August 9 watapimana ubavu dhidi ya Yanga.
Je, Azam Wataliweza Hilii…!?
Fauka na hayo hofu yangu ni moja, je Azam wataiweza vita ya nje ya uwanja? Azam hawako vizuri katika masuala ya nje ya uwanja ukizingatia hawana mashabiki wengi ambao pengine waketia shime na presha kwa timu kufanya vizuri, uchu wa matokeo kwa mashabiki wa Azam ni mdogo pengine sababu ya uchache wao hivyo wachezaji hawauoni msukumo kutoka nje badala yake wanategemea msukumo wa ndani ambao pengine hautoshi kuwasukuma kufikia ndoto kubwa.
NB: USIPIGE KELELE UNAPOKUWA UNAWINDA.