Sambaza....

Vilabu vya Coastal Union ya Tanga, na KMC ya Kinondoni Jijini Dar es salaam jioni ya leo zimepata nafasi ya kupanda ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu ujao.

Coastal Union imekata tiketi hiyo baada ya kuitandika Mawenzi market kwa 2-0 katika mchezo uliofanyikwa kwenye dimba la Jamhuri mjini Morogoro.

 

Mabingwa hao wa soka wa mwaka 1988 walipata bao la kwanza kupitia kwa Raizin Hafidh kunako dakika ya 26, kabla ya kiungo wa zamani wa vilabu vya Simba na Yanga Athuman Iddi “Chuji” kushindikia msumali wa mwisho kunako dakika ya 75, hivyo kujikatia tiketi hiyo ya kurejea ligi kuu ikiwa ni baada ya misimu miwili kupita.

Kwa upande wa KMC inayonolewa na kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Fred Felix Isaya Kataraiya Minziro “Majeshi” wao wameitandika JKT Mlale kwa bao 1-0 likifungwa na kiungo wa zamani wa Simba sc Abdulhalim Humud, katika mchezo uliopigwa kunako dimba la Majimaji mjini Songea.

 

Katika michezo mingine ya kundi hilo Mbeya kwanza wakiwa kwenye dimba Sokoine mjini Mbeya wamepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Dar es salaam, Polisi Tanzania imewalaza wenyeji wao Mufindi kwa mabao 2-1

Matokeo hayo yanaifanya KMC kuongoza msimamo wa kundi “B” kwa alama zao 28, ikuatiwa na Coastal Union yenye alama 26, JKT Mlale alama 25, Polisi Tanzania alama 24, Mbeya kwanza alama 22, Mufindi alama 13, Mawenzi alama 8, huku Polisi Dar es salaam wakisaliwa na alama 5 zikiwafanya kutelemka hadi ligi daraja la pili

 

Sambaza....