Kocha Mkuu wa Rivers United, Stanley Eguma, amefichua kuwa timu yake inakuja na mbinu tofauti dhidi ya Young Africans ya Tanzania katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Rivers watakuwa wenyeji wa mabingwa hao wa Tanzania katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio siku ya Jumapili.
Eguma alisema hayo wakati wa mahojiano ya kabla ya mechi kuwa Rivers United inapanga kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kufika nusu fainali. “Hatutegemei kucheza kama mchezo uliopita, ni michezo miwili tofauti ambayo haifanani,” Eguma aliiambia Daily Post.
“Ninaelewa kuwa Young Africans imeijenga upya timu yake na wanafanya vizuri wakati huu kwenye ligi ya ndani, pia wameongoza kundi lao kwenye kombe la shirikisho.” alisema kocha huyo.
Itakumbukwa kuwa Rivers United iliifunga Young Africans katika mikondo yote miwili ya hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika CAF mnamo 2021.