Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba ndio timu pekee iliyofuzu katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Africa kutoka ukanda huu wa Africa Mashariki na Kati [CECAFA]. Na pia ni klabu mbili pekee kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara zilizofuzu kwa hatua hii wakiungana na Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini.

Simba imefuzu robo fainali ikitokea Kundi C wakiungana na Raja Casablanca baada ya kuwatoa Horoya Fc na Vipers Fc. Simba katika kundi hilo walimaliza wapili wakiwa na alama tisa nyuma ya vigogo Raja.

 

Katika timu nane zilizofuzu robo fainali Mnyama Simba anatarajiwa kukutana na vinara wa kundi kutoka makundi mengine matatu kundi A,B na D baada ya yeye kumaliza nafasi ya pili. Hivyo Simba anatarajiwa kukutana na vigogo hawa Mamelody Sundowns, Wydad Casablanca na Esperence de Tunis. Tuzitazame timu hizi tatu ambazo Simba atakutana na mmoja wapo robo fainali.

Mamelody Sundowns!

Wamemaliza vinara wa Kundi B wakiwa na alama 14 mbele ya Al Ahly na Al Hilal wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja, wakishinda michezo minne na sare mbili pekee. Wamefunga mabao 14 na kuruhusu matatu pekee, wanashika nafasi ya pili nyuma ya Raja kwa timu zilizofunga mabao mengi zaidi.

Mamelody pia katika Ligi yao hawapo vibaya kwani tayari wameshanyakua ubingwa licha ya kuwa na viporo kutokana na ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa. Mpaka sasa wana alama 59 katika michezo 23 waliyocheza na kuongoza Ligi kwa tofauti ya alama 16 na kubeba ubingwa mara ya sita mfululizo.

Mamelody Sundowns

Miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vyema msimu licha ya rekodi yake mbovu kwa miaka ya hivi karibu kwa kushindwa kuvuka robo fainali kwa miaka zaidi ya minne. Endapo Simba itapangiwa Mamelody haitakua mara ya kwanza kwenda katika ardhi ya Afrika Kusini kwani tayari amecheza robo fainali mbili mfululizo nchini humo dhidi ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.

Esperence de Tunis.

Mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika mwaka 2018 wakifuzu kutokea Kundi D wakiwa na alama 11 mbele ya CD Belouzdaid waliomaliza wapili wakati Zamaleck na El Merreck wakishindwa kufuzu. Esperence ndio timu iliyomaliza vinara yenye wastani mdogo wa magoli kwani imefunga mabao 6 na kufungwa manne hivyo wana tofauti ya mabao mawili pekee.

Kwenye Ligi yao ambayo nchini Tunisia inachezwa katika mfumo wa makundi wao wapo nafasi ya pili pili wakiwa na alama 7 nyumba ya Etoile du Sahel wenye alama 9 wakiwa wanagombania ubingwa na uwakili wa Kimataifa.

Esperence de Tunis.

Tangu ilipochukua ubingwa mwaka 2018 bado haijawa tena tishio sana na kama Simba watakwenda Tunisia kucheza nao robo fainali itakua ni mara yao ya kwanza kwa miaka ya hivi karibuni tangu warudi anga za Kimataifa na kufanya vyema.

Wydad Casablanca.

Hawa ndio mabingwa watetezi wa kombe hili baada ya kumfunga Al Ahly msimu uliopita. Wamefuzu kutoka Kundi A wakiwa na alama 13 mbele ya JS Kabyele waliomaliza wapili. Wamefunga mabao 7 na wakiruhusu bao moja pekee.

Kwenye Ligi bado wapo katika nafasi nzuri kwani mpaka sasa wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 42 katika michezo 20 waliyoshuka dimbani.

Wydad Casablanca.

Endapo Simba atapangwa na wababe hawa tayari Mnyama ameshaonja ladha ya Wamorocco kwani ameshacheza na mtani wake Raja Casablanca na kupigwa nje ndani hivyo ni wazi sio eneo zuri kwa Simba haswa ukizingatia ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo.

Sambaza....