Jumapili jioni ya tarehe 19 Yanga wanafunga bao katika kila kipindi mbele ya timu kutoka Tunisia US Monastir mpira unamalizika bao mbili bila na Yanga wanafuzu kwenda robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Jana yake Jumamosi ya Machi 18 Mnyama Simba nae anafuzu kwenda robo fainali mbele ya matajiri kutoka Guinea Horoya kwa kuwafunga mabao saba kwa bila huku mchezaji mmoja akifunga mabao matatu.
Simba na Yanga si tu zimefuzu kwenda robo fainali lakini pia zinafuzu huku wakiwa na mchezo mkononi. Yaani wanaingia katika michezo yao ya mwisho ya makundi kukamilisha ratiba si tena kwenda kusaka ushindi.
Vilabu vyetu vimeonekana kupiga hatua kwa haraka zaidi katika michuano hii mikubwa ya vilabu Afrika na kutufanya sasa tuanze kuona mamba tuliyokua tunayaota kama nchi yanawezekana na sasa tunaishi ndoto zetu.
Awali ilikua nadra kwa vilabu vya Tanzania kushiriki makundi ya michuano hii miwili mikubwa lakini pia hata tuliposhiriki hatukuweza kuvuka hatua ya makundi. Yanga waliwahi kufanya hivi mara mbili mwaka 2016 na 2018, wakati Simba walishiriki makundi mwaka 2003.
Simba ndio waliokua wakwanza kuanza mapinduzi haya mwaka 2018 walipowatoa Nkana na kwenda kushiriki makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoboa mpaka robo fainali. Na tangu hapo ikawa ni kawaida kwa timu za Tanzania kuingia hatua ya makundi ambapo klabu kama Namungo nayo ilifanikiwa kufuzu na kucheza makundi mwaka 2021.
Kwasasa nchi imezoea kutazama vilabu vikubwa vikija nchi kupambana na timu zetu katika michezo ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa na hii ni kutokana na kuimarika kwa vilabu vyetu hivyo kuwa na uwezo wa kupambana na vilabu vikubwa kama Al Ahly, TP Mazembe, Al Hilal, Kaizer Chiefs n.k.
Simba na Yanga si tu kwamba wanatuletea timu kubwa Afrika lakini pia wanatupa uhakika wakupata na ushindi mbele ya vilabu hivyo ambavyo vimepiga hatua kubwa katika soka nchini mwao. Simba imeweza kupata ushindi mbele ya Ahly, Horoya, Asec Mimosa, AS Vita. Hata Yanga wametupa ushindi mbele ya Moalnastir, Mazembe na Africain tena ugenini.
Yote hii ni ishara yakupanda kwa viwango kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika vilabu vyetu na matajiri wakubwa wa nchi. Uwekezaji huu unawafanya kuweza kuwanunua wachezaji kutoka nje wenye uweso mkubwa na kuweza kupambana na vilabu vikubwa.
Pesa za Mo Simba zimewaleta kina Clatous Chama, Luis Miquissone, Meddie Kagere, Sadio Kanoute, Inonga Baka na wengine wengi kama hao wanaoifanya Simba iwe ya ushindani Afrika. Wakati pesa ya GSM imewaleta kina Fiston Mayele, Kenedy Musonda, Djigui Diara, Aziz Ki na wengine wengi.
Sasa Simba na Yanga zinapishana katika viwanja vya ndege vya Kimataifa wakienda kupambana na vigogo wengine Afrika, wakati pia tuna uhakika wakupata mechi nzuri kila weekend pale Kwa Mkapa kama ambavyo mwaka huu tumeona.