Ligi kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite inaendelea kutimua vumbi tena leo baada ya mapumziko mafupi yakumaliza mzunguko wa kwanza.
Ligi hiyo ilisimama baada ya michezo michezo yote tisa ya raundi ya kwanza kumalizika huku Simba Queens wakiwa kileleni na alama 22 wakiwaacha nyuma JKT Queens wenye alama 21 huku Fountaine Gate na Yanga Princess wakishika nafasi ya tatu na nne wakiwa na alama 20.
Simba wanashuka dimbani wakiwa ugenini katika uwanja wa Meja Generali Isamuhyo Mbweni wakikaribishwa na JKT Queens katika mchezo wa kisasi kwani katika mchezo wa raundi ya kwanza Simba Queens walifungwa nyumbani kwao katika Dimba la Mo Arena kwa mabao mawili kwa moja.
Mchezo huu pia utaamua ni nani atakaa kileleni kwa Simba wanaongoza kwa tofauti ya alama moja pekee, Simba wana alama 22 na JKT Queens wana alama 21 hivyo ushindi kwa Simba wataendelea kujikita kileleni na ushindi wa JKT watawashusha Simba kileleni na kukaa wao.
Yanga Princess wao watakua na kibarua dhidi ya Fountaine Gate Princess katika Dimba la Jamuhuri Morogoro. Katika mchezo wa kwanza Yanga Princess walikubali kichapo cha bao moja kwa sifuri katika uwanja wao wa nyumbani Uhuru.
Mchezo huo unategemewa kuwa na ushindani mkubwa kwani timu hizo zinafuatana katika nafasi ya tatu na nne na wote wakiwa na alama 20 katika msimamo wa Ligi.