Pappy Kabamba Tshitshimbi “Rasta” kiungo maridhawa wa chini kipenzi cha wanajangwani. Utawaambia nini mashabiki wa Yanga kuhusu Pappy wakuelewe?
Moja ya viungo bora mpaka sasa kwenye vodacom premier league, huku tukielekea kuhitimisha leo raundi ya raundi ya kwanza ya VPL. Ameonyesha uwezo mkubwa wa kukaba, kupiga pasi, kuendesha timu na kusaidia mashambulizi lakini pia kujaribu kufunga kwa mashuti makali pale inapobidi.
Amethibitisha Uwezo Wake Kikamilifu
Kwa mara ya kwanza alianza kuonekana na kutamkwa na Watanzania pale Azam Complex Chamanzi alipokuja na Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa Kombe la shirikisho Africa.
Tangu alipoanza kuitumikia Yanga kwenye mechi ya ngao ya jamii dhidi ya Simba na mechi nyingine za ndani za ligi hakuna alieonyesha wasiwasi juu ya uwezo wa ”Mkongomani” huyu. Ameendelea kujipambanua na kuonyesha jinsi gani ni kiungo aliekamilika katika kikosi cha Yanga.
Aliletwa Yanga kuja kumaliza tatizo la kiungo mkabaji ambapo toka aondoke Athumani Idd ”CHUJI” na Frank Dumayo ”CHUMVI” na mara kwa mara kuwakosa Jonas Gerald Mkude wa Simbasc na Himid Mao Mkami wa Azamfc Yanga ilionekana kuteteteraka. Hivyo kumpata Pappy kuja kujenga ”partnership” na Kamusoko ni ushindi kwa Yanga katika eneo la kiungo.
Ameonyesha Ni Mchezaji Wa Mechi Kubwa.
Mpaka sasa hajafunga goli lolote kwenye VPL lakini haifanyi kumkataa kiungo huyu kutoka kwa jirani yetu bwana Joseph Kabila.
Toka mechi yake ya kwanza ya kimashindano akiwa na jezi ya Yanga aliyocheza kwenye ngao ya jamii dhidi ya mahasimu wao Simbasc hajawahi kukosea kwenye mechi kubwa kama hizi. Akicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Simbasc uwanja wa Taifa alifanya kazi kubwa katikati ya uwanja kiasi cha kuwapa tabu viungo wa timu pinzani haswaa wakiongozwa na Haruna Niyonzima. Aliweza kuipa timu balance na kupora mipira na kuwalazimisha viungo wa Simba wacheze anavyotaka yeye.
Mwisho alipiga penati maridhawa na kumtesa kipa wa Simba Aishi Salum Manula, japo Yanga alipoteza mechi kwa mikwaju ya penati.
Mechi yake ya pili ilikua dhidi ya Simbasc tena katika VPL Uwanja wa Uhuru ambapo mchezo uliisha kwa sare ya bao moja kwa moja.
Utake nini tena kwa kiungo Pappy kwenye mechi dhidi ya mtani kwa kiwango kile alichokionyesha? Kutimia kwenye kukaba, kusukuma timu juu, kupiga pasi za uhakika na mashuti ya mbali. Kwenye mchezo huu mara mbili alikaribia kufunga kama sio umahiri wa kipa wa Simba Aishi Manula. Aliweza kupiga mashuti mara mbili tena kwa ustadi mkubwa akiwa nje ya kumi na nane ya eneo la Simba.
Mchezo wake wa tatu ni dhidi ya Azamfc katika uwanja wa Chamanzi complex katika mechi ya mwisho ya kukamilisha raundi ya kwanza. Stephano Kingue Sure Boy walishindwa kabisa kufua dafu kwa Mcongo huyo aliyeanza kama kiungo mshambuliaji akisaidiwa na Said Makapu katika kiungo cha ulinzi. Pappy aliimudu presha ya Azam waliokua nyumbani na mashabiki wao na kumpoteza kabisa Sure Boy eneo la kiungo. Hata pale kocha wa Azam alipoamua kumuongeza Salmin Hoza katika kiungo cha Azam lakini bado Pappy alicheza kwa maelekezo ya mwalimu na kuweza kuwadhibiti Azam.
Lakini pia akaisaida timu yake kupata ushindi mbele ya Azam na kuweza kutoa pasi ya bao kwa Gadiel Michael Mbaga.
Pappy Kabamba Tshitshimbi tunakusubiri tuone huu moto pia katika michuano ya Kimataifa mwezi ujao pale ambapo Yanga itarudi tena anga za kimataifa katika Klabu Bingwa Africa.