WANAMUZIKI/ WAIMBAJI WA NYIMBO ZA KUSIFU TIMU ZETU ZA MPIRA WA MIGUU IMBENI NYIMBO ZITAKAZODUMU MILELE. Anandika Sady.
Binafsi niseme wazi tu kwamba mimi ni miongoni mwa watu wanaopenda sana muziki, hasa muziki mzuri.
Bila kujali muimbaji katumia lugha gani na bila kujali kama ninaelewa au sielewi kilichoimbwa ili mradi sio matusi basi kama ni muziki ama wimbo mzuri mi nitaupenda, kuucheza na kuusikiliza pia.
00:00
Leo nataka nije kwa hawa wanamuziki na waimbaji wetu hapa Tanzania. Hawa ambao hutuimbia nyimbo kwa ajili ya kuhamasisha na kuleta burudani kwa soka letu hasa vilabu hivi pendwa vya Simba na Yanga.
Kumekuwa na nyimbo nyingi sana zimeimbwa na tumezifurahia hasa kwa midundo na sauti za waimbaji wetu mahiri ambazo zimepangiliwa vema na kutupa “vibe” pale zinapopigwa.
Nimefuatilia kwa muda mrefu sasa na bado naona makosa ya utunzi yanaendelea siku hadi siku, nyimbo nyingi zilizoimbwa ni nyimbo za msimu mmoja tu. Haziwezi kutumika kwa msimu mwingine au hata nusu ya pili ya msimu kwasababu zinakosa maana na mantiki kwa timu iliyoimbiwa wimbo huo.
Wanamuziki na waimbaji wetu nadhani labda hawajui vizuri soka na wachezaji, waimbaji na watunzi wa nyimbo hizi wamekuwa wakiimba nyimbo zao kwa kutaja majina ya wachezaji ama viongozi wa timu husika kwenye nyimbo zao. Wamekuwa wakifanya hivi sijui ni makusudi au kwa kutokujua kwamba wachezaji huwa hawana timu? Sijui wanajua kwamba mchezaji leo anaweza kuwa Simba na dirisha dogo la usajili mwezi Januari akwa Yanga au Namungo? Hiviwanajua hiki kweli?
Kwanini wimbo wako mzuri ukose maana sababu tu umemtaja mchezaji ambaye hivi sasa hayuko na timu uliyowaimbia wimbo huo? Mbaya zaidi unakuta sasa mchezaji huyo katoka upande wa Simba kaenda Yanga ambao ni mahasimu.
Leo tunaancha kuenjoy muziki wenu mzuri kisa tu majina, leo shabiki wa Simba ataacha kusikiliza na kuucheza wimbo wa Diamond Platnumz sababu Manara katajwa mule. Kesho na keshokutwa wimbo wa ni yuleyule utaachea kusikilizwa na mashabiki wa Yanga sababu Ntinzonkiza katajwa na labda yupo timu pinzani wa Yanga kwa wakati huo maana hayupo na Yanga hivi sasa.
Ushauri wangu kwenu ni kwamba, kwenye tungo zenu mjitahidi kuitaja na kuisifu timu kwa mafanikio yake au namna ilivyo bila kuihusisha na wachezaji tena wachezaji wenyewe wamesajiliwa kwa mikataba ya miezi 6 tu. Fanyeni nyimbo ambazo zitaishi milele na milele, mbona miziki ya miaka ya 70 na 80 au hata nyuma ya hapo tunaisikiliza sisi wa kizazi cha sasa!?
Uchambuzi na: Sady A. Mwang’onda.