Sambaza....

Ule mchezo wakitamaduni, mchezo watani wa jadi, mchezo mkubwa Afrika Mashariki na Kati Simba na Yanga hatimae umefika baada ya kusubiriwa kwa takribani miezi saba tangu mechi ya mzunguko wa kwanza ilipochezwa.

Ni April 30 katika dimba la Benjamin Mkapa Temeke Dar es salaaam Yanga atamkaribisha Simba katika mchezo wa raundi ya pili baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa suluhu.

Yanga wapo kileleni wakiwa na alama 54 wakifwatiwa na watani wao wenye alama 41, Yanga wanaongoza Ligi tofauti ya alama 13 tena bila kufungwa hata mchezo mmoja. Ushindi katika mchezo huu kwa Yanga maana yake ni kujihakikishia ubingwa kwa asilimi 100.

Hassan Dilunga (kushoto) akiwania mpira na Djuma Shaban.

Kikosi Yanga!

Tukianza na mwenyeji Yanga, Profesa Nasraden Nabi hatokua na kazi kubwa ya kubadili kikosi chake kutokana na jinsi alivyokitengeneza msimu huu na jinsi ambavyo amekipanga kikosi chake na kupata matokeo katika michezo yake ya mwisho.

Nabi amekua akitumia mfumo wa 4:2:3:1 ama 4:3:3 kutokana na aina ya mpinzani. Lakini kuelekea katika mchezo wa Simba ni wazi atatumia 4:2:3:1 haswa ukichagizwa na urejeo wa viungo wake tegemeo Feisal Salum na Khalid Aucho. 

Khalid Aucho (kushoto) na Feisal Salum (kulia).

Katika eneo la ulinzi ni wazi hakutokua na mabadiliko makubwa ambapo Djugui Diara atakua langoni huku walinzi wa kati wakitarakiwa kuwa ni nahodha Bakari Mwamnyeto na Yanick Bangala wakati upande wa kushoto ni Kibwana Shomary na ulinzi wa kulia utategemea afya ya Djuma Shabani, kama atakua fiti atasimama eneo lake la ulinzi wa kulia lakini kama atakua katika sintofahamu eneo hili litakua chini ya Dickson Job. 

Katika eneo la kiungo wa ulinzi urejeo wa Khalid Aucho na kiwango bora cha Salum Aboubacar ni wazi watakabidhiwa eneo hilo mbele ya Zawadi Mauya na Yanick Bangala ambae mwalimu ataamua kumshusha chini katika eneo la beki wa kati.

Salum Aboubacar “Sure Boy” akipiga mpira mbele ya kiungo wa timu pinzani.

Kwa upande wa viungo washambuliaji Feisali ni dhahiri shahiri atakua namba 10 mbele ya viungo wawili Sure Boy na Khalid Aucho halafu upande wa winga ya kushoto atasimama Saidoo Ntibazonkiza na winga ya kulia ni Jesus Moloko. Urejeo wa Saidoo na kasi ya Moloko unamfanya mwalim aamue kuanza nao hao na kuwaacha benchi Chico Ushindi, Denis Nkane na Dickson Ambundo ambao watatumika kama plan B wakitokea benchi.

Katika eneo la mshambuliaji wa mwisho yaani “main man” pasi na shaka uchaguzi ni mwepesi tu, ni Fiston Kalala Mayele ndie atakaepewa nafasi ya kwenda kuukwamisha mpira wavuni mbele ya kina Inonga na Onyango. Ni wazi Heriter Makambo na Crispine Ngushi watakaa katika benchi na kumtazama kinara wa mabao akifanya yake.

Kikosi cha Simba!

Baada ya kutolewa katika kombe la Shirikisho Afrika ni wazi kocha Pablo Franco ana kazi kubwa yakujenga saikolojia ya wachezaji wake ili kuwarusha mchezo mchezo kuelekea mchezo huu mgumu ambao huenda ukaamua hatma yake  katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Pablo Franco amekua akitumia mfumo wa 4:3:3 ambao hutegemea katika kasi ya Morrison, Banda na Pape Sakho kupelekea mashabmulizi kwa mpinzani. Mara chache akitumia mfumo wa 5:4:1 haswa katika mchezo dhidi ya Orlando Pirates na RS Berkane ugenini. 

Katika mfumo wa 4:3:3 ni wazi Pablo hatotaka kifumua ukuta wake na kuweka watu walinzi wake walewale wanne. Henock Inonga ata”double” na Joash Onyango huku Pascal Wawa akisuburi nje, kwa upande wa mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Mohamed Hussein wataziba upande wa kulia na kushoto wakati mdogo wao Israel Mwenda akikaa nje kama “Plan B”.

Katika eneo la kiungo licha upana wa eneo hilo lakini hakuna namna Pablo Franco atavunja “double pivot” yake ya Jonas Mkude na Sadio Kanoute “Mkuki”, wawili hawa wamekua na maelewano mazuri katika eneo la kiungo la Simba. Hivyo Mzamiru Yassin na Thadeo Lwanga watakua katika bechi wakitazama mchezo wakisubiri lolote litakalotokea kiwanjani.

Sadio Kanoute “Mkuki” akichukua mpira mbele ya wachezaji wa Asec Mimosa

Pablo Franco pia ni wazi atamtumia Clatous Chama katika eneo la katikati kuinganisha timu. Chama hajacheza mechi ya ushindani kwa takribani wiki mbili kutokana na kutotumika katika mchezo wa shirikisho. Chama ana kubwa mbele ya Rally Bwalya ambae amekua hana kiwango cha kueleweka. 

Kwa upande wa eneo la ushambuliaji mwalimu wa Simba mbinu zake za kulishambulia lango la mpinzani zipo katika kasi na mikimbio ya kina Morrison na Pape Sakho ambao husimama pembeni ya mshambuliaji wa kati Cris Mugalu. Katika mpango kazi wa Pablo hupenda kumsimamisha Cris Mugalu kama mshambuliaji wa kati mwenye uwezo wa kupambana na mabeki lakini pia kurahisisha kazi kwa kina Sakho na Morisson ambao hutokea nyuma yake. 

Sambaza....