Wazir Junior ni jina ambalo limeonekana sana kwenye habari za michezo hapa nchini kwenye msimu uliopita baada ya yeye kufanya vyema kwenye ligi kuu.
Wazir Junior alikuwa mshambuliaji tegemeo wa klabu ya Mbao FC iliyoshuka daraja msimu uliopita ambapo alimaliza msimu akiwa na magoli 14 nyuma ya mfungaji bora Meddie Kagere.
Klabu ya Yanga imemsajili Wazir Junior na rasmi msimu ujao atakuwa kwenye jezi ya njano na kijani. Akizungumza na mtandao huu wa kandanda.co.tz Wazir Junior ameahidi moto ule wa Mbao FC utaendelea akiwa Yanga.
“Kwanza kabisa namshukuru mwenyezi Mungu ni kitu ambacho nilikuwa nakitamani kwa muda mrefu. Nilikuwa napigana ili siku moja nije kuchezea Yanga , nawaahidi mashabiki wa Yanga moto ule ule wa Mbao utaendelea nikiwa Yanga”- alisema Wazir Junior.
Alipoulizwa ipi mipango yake msimu ujao alisema kuwa amepanga msimu ujao atakuwa mfungaji bora wa ligi kuu na amejipanga kupambana na washambuliaji kama Meddie Kagere.
“Mshambuliaji kazi yake ni kufunga tu na mimi nimejipanga kufunga tu hakuna kitu kingine. Mimi lengo langu ni kuwa mfungaji bora. Kuhusu msimu uliopita sikupata mechi nyingi lakini msimu huu nimejipanga kupata mechi nyingi na kuwa mfungaji bora”- alisema Wazir Junior