Wekundu wa Msimbazi Simba katika mchezo dhidi ya Namungo fc wamekabidhiwa kombe lao lao la ubingwa baada ya kuibuka mabingwa katika msimu huu wa 2019/2020. Simba ilifanikiwa kujihakikishia kubeba taji lake baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prisons jijini Mbeya.
Kwa ubingwa wa msimu huu maana yake Simba wamelinyakua kombe la Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo. Simba wametwaa ubingwa kwa msimu wa 2017/2018, 2018/2019 na msimu huu wa 2019/2020.
Simba wamenyakua ubingwa mbele ya washindani wao wakuu Azam fc na Yanga ambao kwasasa wanapambania nafasi ya pili katika Ligi na Namungo fc.
Ukitazama jinsi Simba walivyotwaa taji la tatu mfululizo huoni dalili za wao kuukosa tena ubingwa wa msimu ujao na hii ni kutokana na sababu zifuatazao:
1. Kikosi cha Simba kimesheheni.
Simba imetwaa ubingwa ikiwa na michezo sita mkononi na si kwa bahati mbaya bali ni kweli walidhamiria kufanya hivyo, ukitaka kujua hilo tazama wachezaji wanaounda kikosi chao. Simba inawechezaji imara karibu katika kila eneo la uchezaji, wanaokaa njee na walioanza na hata waliokaa jukwaani bado ni imara ambao katika vikosi vingine wanaanza.
Sehemu pekee inayoonekana kukosa usawa ni eneo la ulinzi. Lakini katika maeneo mengine yote yametimia, kwa mfano eneo la kiungo wa pembeni na kiungo wa katikati karibia nafasi moja ina wachezaji wawili mpaka watatu wenye uwezo mkubwa. Deo Kanda, Hassan Dilunga, Fransis Kahata (Winga ya kulia). Luis Miquissone, Miraj Athuman, Shiza Kichuya (Winga ya kulia). Hilo ni eneo moja tu lakini tazama pia eneo la katikati ya uwanja kuna Jonas Mkude, Fraga Viera, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Sharaf Shiboub na Clatous Chama.
2. Usajili wa uhakika.
Kwa misimu ya hivi karibuni Simba imeonekana kufanya usajili wa uhakika haswa kwa nyota wanaotoka nje ya nchi. Meddie Kagere, Clatous Chama, Francis Kahata na Luis Miquissone hao ni baadhi tu ya nyota ambao Simbe imelamba dume kwenye sajili zao. Ni wachezaji wachache ambao Simba unaweza sema ilikosea kama wale Wabrazil lakini wengine wote wameonekana kuingia kwenye mfumo na kuisadia Simba.
Hiyo imekua tofauti kwa wapinzani wao wa Yanga na Azam kwa miaka ya hivi karibuni wamekosa bahati ya kupata wachezaji wazuri haswa wa kigeni.
3. Yanga na Azam dhaifu.
Wapinzani wa Simba kwenye ubingwa ni Yanga na Azam fc lakini kwa miaka hii mitatu wameonekana kushindwa kutoa upinzani sahihi kwa Simba. Ni dalili mbaya kwa klabu kuchukua ubingwa tena kwa tofauti ya alama nyingi na michezo kibao mkononi kutoka kwa wapinzani wake wakuu. Yanga na Azam wameshindwa kua wapinzani halisi katika mbio hizi hivyo kuzidi kuipa nafasi Simba ya kutawala zaidi na zaidi kama hawatobadilika.
4. Tamaa ya mafanikio ya Kimataifa.
Simba imekua ikiweka wazi hamu yake ya kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika. N hii itawasaidia katika nyanja mbili kuendelea kutwaa ubingwa wa VPL.
Kwanza, ili kushiriki michuano ya Kimataifa ni lazima uwe bingwa nchini kwako, hivyo Simba ili kuweza kufanikiwa Kimataifa lazima waendelee kunyakua ubingwa wa ndani. Hii itaifanya Simba kuendelea kulitolea macho taji la Ligi Kuu Bara na kuendeleza ubabe wake.
Pili, ili kufanikiwa Kimataifa lazima uwe na nyota wakubwa Barani Afrika hivyo ni lazima Simba wafungue pochi ili kunasa nyota wakubwa wa kuweza kupambana na Zamalek, Tp Mazembe na Mamelodi Sundown.
Kwa usajili huo maana yake ni wazi Simba itashiriki Ligi Kuu Bara ikiwa na wachezaji wakubwa Afrika ambao watarahisisha kazi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
5. Uchumi wa Vilabu vingine.
Ni wazi Simba ipo vizuri kwenye maswala ya fedha kuliko kilabu chochote nchini na Afrika Mashariki. Kambi nzuri, malipo mazuri,usafiri mzuri na viwanja vizuri kabisa vya mazoezi. Ukivitazama vilabu vingine ni ndoto kufika alipo Simba ukiwatoa Azam fc na Yanga.
Hivyo ni ngumu kwa vilabu kama Kagera, Mtibwa, Lipuli au Coastal Union kuweza kuibuka na kushindania ubingwa wa Ligi kama ambavyo aliwahi kufanya Leicester City katika EPL. Ni ngumu kutokea kwa maajabu kama haya, ni wazi sasa Simba ataendelea kutesa katika kutwaa ubingwa wa Bara kama vilabu vitaendelea kushiriki Ligi kwa kutegemea udhamini wa Vodacom na Azamtv.