Hakuna ufanano wowote uliowahi kuwekwa kwenye akili za wanadamu wowote. Mungu aliona hiki ndiyo maana hakuweka ufanano wa mawazo kwenye akili zetu. Ushawahi kujiuliza ingekuwa vipi kama kila mtu angekuwa anawaza sawa na mwenzake ?. Hapana shaka kusingekuwepo na maendeleo ndani ya jamii.
Mwanzo wa upatikanaji wa maendeleo ni pale kunapokuwepo na mkinzano wa mawazo, mkinzano ambao huleta wazo moja ambalo ni bora kwenye maendeleo. Kila mtu ana namna anavyotazama mambo, ni haki yake ya kimsingi kabisa. Na ndiyo maana kuna mawazo mengi sana ambayo hutoka kila mara timu zetu zinapofanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa.
Wengi wanatamani sana mafanikio, na wengi wanafikiria sana mafanikio kwenye mpira wetu ndiyo maana kila tukipoteza huwa tunaumia sana kwa sababu tu sisi hutamani mafanikio ndani yetu. Kuna mengi sana huwa yanazungumzwa, utasikia huyu akisema tufukuze kocha. Ushawahi kujiuliza ni kocha yupi ambaye ashawahi kutupa mafanikio tunayoyatamani ?
Ushawahi kujiuliza ni makocha wangapi ambao tushawahi kuwafukuza mpaka sasa hivi na kuleta makocha wapya?, hao makocha wapya ni yupi ambaye tuliridhika naye ?
Tuachane na kocha turudi kwenye wimbo ambao kila uchwao huwa tunauimba. Wimbo wa kurudi kwenye misingi.
Kila mtu utamsikia turudi kwenye msingi. Kitu ambacho ni sahihi kabisa, na ndicho kitu ambacho ni dawa katika maendeleo ya mpira wetu.
Na kitu hiki kinahitaji uwekezaji wa muda mrefu ili kufikia mafanikio. Kuwekeza kwa muda mrefu kunahitaji uvumilivu.
Uvumilivu ambao tunatakiwa kuwa nao wakati ambao timu yetu ya taifa inaendelea kushiriki michuano ya kimataifa, hapa ndipo swali ambalo tunatakiwa kujiuliza kwa pamoja, ni kipi tukifanye wakati ambao tunasubiri kujenga misingi ya mpira wetu ?
Kwangu mimi naona ni bora tuwekeze nguvu na akili zetu katika kuwafukuza kina Ibrahim Ajib na kuachana na kasumba za kuwekeza nguvu za kumfukuza Emmanuel Amunike.
Kama ambavyo wengi wetu tunavyosema kuwa michuano ya Afcon ya mwaka huu tumeenda kujifunza na siyo kushindana. Basi kuna vitu ambavyo tunatakiwa kuvichukua kama fundisho.
Mfano , jana wakati tunacheza na timu ya taifa ya Senegal, kikosi chao kilikuwa kimesheheni wachezaji wengi ambao wanacheza katika vilabu vya nje ya nchi yao.
Wao wamefanikiwa katika eneo la kuuza bidhaa inayoitwa wachezaji nje ya nchi. Hapa ndipo tunapotakiwa kuanzia kwa sasa wakati tunasubiri matunda ya msingi wa soka yatulipe.
Tuwekeze nguvu ya kuwafukuza hawa wachezaji wetu waende kucheze ligi za nje. Tukiendelea kufurahia kuwaona kina Ibrahim Ajib wakicheza hapa nchini tutakuwa tunajidanganya na hadithi za kuendelea kupata mafanikio kwenye mpira wa miguu.