Miezi mitatu imepita bila kuwa na Ruge Mutahaba. Gwiji katika masuala ya biashara ya burudani.
Huwezi kutenganisha ubunifu wa biashara ya burudani na Ruge Mutahaba. Ni vitu ambavyo vilizaliwa pamoja, vikaishi pamoja, vikakua pamoja na inawezekana kabisa vimekufa pamoja.
Ruge alihakikisha anatembea na pacha wake mkubwa wa kuitwa ubunifu katika biashara ya burudani.
Hakutaka kumuacha kabisa na kwa pamoja wakang’ang’aniana na kuwa marafiki, marafiki ambao waligeuka kuwa mapacha wanaofanana kabisa.
Ndipo hapo ukawa mwanzo wa kumweheshimu Ruge Mutahaba. Ukawa mwanzo kwetu sisi kuumia kipindi tuliposikia ametutoka.
Tuliumia kwa sababu tu kuna darasa kubwa ambalo limebomoka na ndani yake alikuwepo mwalimu wetu mkubwa.
Mwalimu ambaye aliangalia kila kitu katika jicho la kibiashara. Mwalimu ambaye aliamini chochote kinachofanyika hapa duniani ni biashara.
Kwa bahati mbaya sana hili darasa lilibomoka ghafla na matofali yake yakatumika kutoa uhai wa mwalimu wetu huyu bora kuwahi kutokea.
Inawezekana kabisa leo hii Ruge Mutahaba tusingemkumbuka kwa chochote kile kama asingeamua kuangalia kitu alichokuwa anakifanya kwa jicho la kibiashara.
Hapa ndipo mzizi mkubwa wa kumbukumbu zetu kwa Ruge ulipoanzia. Na hapa ndipo ulikuwa mwanzo wa Ruge kukaa katika mioyo yetu.
Na hapa ndipo utofauti wa Ruge na Azam FC unapoanzia. Inawezekana kabisa Azam FC wapo hapo walipo kwa sababu hawajaitazama hii klabu kama bidhaa.
Ushawahi kujiuliza kwanini Azam FC mpaka sasa hivi haina mashabiki wake halisi tofauti na kuwa na mashabiki ambao ni rangi mbili ?( kwamba mwili uko Azam FC na Moyo uko Simba au Yanga).
Wakati inakuja Azam FC niliamini hii timu itakuwa ya kizazi kipya, kizazi anbacho kitakuwa kinaipenda Azam Fc na kuondokana na mnyororo wa kurithi kuzipenda Simba na Yanga.
Lakini kwa bahati mbaya sana walishindwa kupata mashabiki wapya wa kwao kabisa. Hakukuwepo na mpango mkakati mzuri wa kuwafanya vijana wadogo hawa kuipenda Azam FC.
Hawa ndiyo walitakiwa kutengenezwa kama bidhaa yao. Hawakutakiwa kuwafikiria watu wazima ambao mioyo yao tayari walikuwa wameshawekeza kwa Simba na Yanga.
Walitakiwa kufirikia kizazi hiki cha 1996 kwenda mbele. Kizazi ambacho hutamani kujiingiza katika kupenda kitu kipya. Kibiashara hiki kizazi hupenda kujaribu kiti kipya kila uchwao.
Na Azam FC ilikuwa bidhaa mpya, bidhaa ambayo ingewekeza sababu ya hiki kizazi kuipenda na kujenga himaya yao binafsi ya mashabiki, lakini Azam FC walishindwa kwenye hili.
Kwanini walishindwa ?, kwa sababu tu Azam FC haionekani kama bidhaa mbele ya watu ambao wanaiongoza.
Wanaiona kama kitu ambacho kipo kwa ajili ya kujifurahisha tu. Hawaijali bidhaa hii kama bidhaa zingine.
Hawaipi nafasi ya kuitangaza vizuri bidhaa hii ili iwe katika masikio ya watu wengi, kitu ambacho kingesaidia sana kupata wateja halisi wa bidhaa hii.
Kuna kitu kimoja ambacho Ruge Mutahaba aliwahi kukisema. “Unapofanya vizuri, usisubiri kusifiwa , kama una nafasi ya kujisifia jisifie uwezavyo”.
Hiki kitu unaweza ukakiona cha kiswahili lakini kibiashara kina nafasi kubwa sana katika kukuza bidhaa yako.
Kwanini nasema hivo ?, kipindi bidhaa yako inapofanya vizuri ukaamua kuisifia kwa kuonesha mazuri ya bidhaa yako unajenga vitu viwili.
Cha kwanza unajenga matamanio kwa wateja kuitumia bidhaa yako , watavutiwa na jinsi unavyoisifia na mwisho wa siku watashawishika kuja kuinunua.
Pili, unajenga uaminifu kwa wateja. Bidhaa yako itaanza kuaminiwa kwa sababu umeonesha ubora wa bidhaa yako.
Kwa kifupi kusifia bidhaa yako kipindi inapofanya vizuri unatengeneza wateja wapya na kuwafanya wateja wa zamani waendelee kubaki kwenye bidhaa yako.
Leo hii Azam FC wameshinda treble. Mafanikio makubwa sana msimu huu kushinda ( Kagame FC, Mapinduzi FC na Kombe la chama cha soka cha TFF).
Hiki ni kitu kikubwa sana lakini cha kusikitisha hakionekani kama ni kitu kikubwa kuanzia ndani ya timu mpaka nje ya timu.
Ndani ya timu wenye timu hawajivunii hiki walichokipata. Hawataki kutoka nje na kukitangaza kwa nguvu.
Hawataki kujisifia kwa haya mazuri ambayo wamefanya. Hawataki kabisa kila saa kuliambia sikio la kila mwana soka kuwa Azam FC imeshinda treble.
Mwisho wa siku Azam FC itakosa mashabiki wapya ambao watavutiwa na mafanikio haya makubwa ambayo yanaonekana madogo.
Hiki ndicho kinachouma, treble inaonekana kitu cha kawaida na Azam FC hawaumizwi na hiki kitu kabisa, Azam FC hawana timu ya masoko na chapa ya klabu?
Kwanini hawafikirii kuiuza Azam FC kwa kupitia haya mafanikio?, au hawayaoni kama ni mafanikio? Au hawaoni Azam FC ni bidhaa? Ndipo hapo ninapomkumbuka Ruge aliyeamini mafanikio huja kipindi unapotazama kitu unachokifanya kwa jicho la kibiashara.