Sambaza....

Ni moja ya vitu ambavyo vinaumiza sana, na ndivyo vitu ambavyo humfanya mtu atamani vitu vingi katika akili yake.

Akili yangu ilikuwa inatamani vingi sana kwenye mechi ya jana. Mechi ya kihistoria , mechi ambayo kutokea tena ni kwa nadra.

Ndiyo mechi ambayo binafsi niliona mechi ya kutokea kwa John Bocco lakini sidhani kama matamanio yangu yatakuwa sahihi.

Matamanio yangu yatakuwa yamefunikwa na shuka jeusi linaloitwa umri. Hili ni shuka zito sana ambalo huwezi kuliondoa hivi hivi.

Ndilo shuka ambalo lilikuwa linaziba uzuri wa John Bocco na ndilo shuka ambalo linafanya matamanio yangu yasiwe na uhakika na hiki ninachokitamani.

Natamani sana hii mechi ingekuja kipindi cha nyuma. Kipindi ambacho John Bocco akiwa na umri mdogo. Natamani sana.

Bocco kushoto akielekeza jambo

Nahisi hiki ndicho kingekuwa kipindi kizuri kwa John Bocco kuliko Jana. Nahisi kabisa kingekuwa kipindi ambacho Sevilla wangeenda moja kwa moja na John Bocco.

Huyu ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa mechi ya Jana. Mchezaji ambaye alifunga goli 2 na kutoa pasi ya mwisho ya goli.

Kwa hiyo alihusika katika magoli matatu (3) kati ya magili manne (4) ambayo jana Simba walifanikiwa kufunga.

Alikuwa kiongozi imara na bora katika mechi ya jana. Alifanikiwa kuwaongoza wanajeshi weusi ambao walikuwa wanapambana na wanajeshi weupe.

Hiki nacho kilikuwa kigezo cha pili ambacho kingempa sifa kubwa ya kuchukuliwa na Sevilla katika mechi ya Jana.

Mchezaji hatari kiongozi, hakuna timu ambayo haiitaji mchezaji bora ambaye anasifa za ziada ya kuwa kiongozi.

Vyote hivi vilikuwa vinampa nguvu kubwa sana John Bocco katika mechi ya jana dhidi ya Sevilla, lakini kilichokuwa kinamwangusha ni umri tu.

Nahisi Sevilla walitamani kumchukua jana lakini kikwazo kikubwa kilikuwa umri, na ndicho kitu ambacho kilimkwamisha Jana.

Mechi ya jana ilikuja wakati ambao jua la jioni likiwa linaelekea kuzama kwenye utosi wa John Bocco kitu ambacho sikutamani kabisa kitokee kwa John Bocco.

Sambaza....