Sambaza....

Hapana shaka hii ni moja ya klabu ambayo ina mashabiki wengi sana hapa nchini Tanzania. Ushawahi kuishuhudia Yanga kila ikikanyaga kwenye ardhi ya mkoa wowote ?

Mkoa husika kwa siku hiyo huwa kama kuna sikukuu maalumu. Sikukuu ya Yanga , sikukuu ambayo hupambwa kwa rangi ya njano na kijani.

Na kama kungekuwa na uwezekano wa kubadilisha rangi ya chakula basi hata ugali kwa siku hiyo ungepikwa kwa rangi ya njano na kijani.

Haya ni mapenzi makubwa sana kwa mashabiki. Wanaipenda sana timu yao kupitiliza. Huwa ni mahaba makubwa sana ambayo ni mara chache sana kuyaona ya kitokea tena kipindi hiki ambacho mapenzi siyo kitu cha muhimu kwa wanadamu.

Viwanja hufurika kwa ajili ya kuiona Yanga kwa siku husika. Mashabiki hutamaraki, huvalia fulana zao za kijani na njano.

Hubeba vuvuzela, ngoma na wakati mwingine ngozi zao za mwili hupakwa kwa rangi ya njano na kijani. Hii yote ni kuonesha mapenzi ya dhati kwa timu.

Kuna wakati huwa nafikiria kuwa kama kungekuwa na uwezekano wa kubadilisha rangi ya damu basi mashabiki wa Yanga wangeweza kuibadili rangi yao kuwa ya njano na kijani.

Hii yote ni kwa sababu tu ya Yanga. Na kuna wakati mashabiki hawa hawa wanaposikia timu imekwama kiuchumi wao husimama.

Huhakikisha chochote kitu ambacho wanacho mfukoni mwao wanakihamisha na kukipeleka kwa Yanga ili tu wachezaji wasiteseke.

Hii ndiyo huwa furaha yao kubwa. Kuiona Yanga ikicheza na kupata ushindi. Tena mapenzi yao ya ajabu kabisa, hawatazami uzuri wa mwanamke wanachotaka ni kama mwanamke anaweza kuzaa.

Ndiyo maana huwezi kukuta shabiki wa Yanga akilalamika timu yake inacheza mpira mbovu. Kwa wao uzuri wa mpira hauna maana, ila ushindi ndicho kitu kikubwa kwao.

Ni ngumu kupata mapenzi ya namna hii kwenye dunia hii ya ajabu. Dunia ambayo sura na pesa zimetangulizwa mbele.

Huwezi kupendwa kama huna pesa , basi ukikosa pesa uwe hata na muonekano. Lakini mashabiki wa Yanga wanaishi kwenye dunia yao ya kipekee.

Wanaipenda Yanga ambayo haina pesa na kuna wakati wanaipa Yanga pesa katika mfumo usio rasmi. Haiishii hapo tu, wanaipenda Yanga ambayo haichezi mpira wa kuvutia.

Hiki ndicho kitu cha ajabu na ƙitu kigumu kueleweka moja kwa moja kuwa kwanini wanaipenda hivi Yanga?. Ni upendo wa Agape?

Kama ni upendo wa Agape viongozi wanautumiaje upendo huu ili kuinufaisha timu ?. Hivi viongozi hawaoni kuwa wana mtaji mkubwa wa kuwa na mashabiki ambao wanaipenda timu yao kwa dhati?

Kwanini wasiwatengenezee mazingira ambayo ni bora kwa ajili ya hawa mashabiki kutoa pesa zao kwa njia ambayo ni rasmi ili Yanga inufaike na mashabiki wanufaike?

Kwenye dunia hii ya kibiashara hakuna mtu anayependa kutoa pesa yake mfukoni bila yeye kupata chochote kitu baada ya kutoa hiyo pesa yake.

Tuko katiƙa dunia ya kipebari. Hatuko kwenye dunia ya kiujamaa. Tumeshapita hiyo dunia muda mrefu sana.

Faheem, moja ya mashabiki wa Yanga

Tusipende kuishi kiujmaa. Tuishi kibepari kama tunataka kufanikiwa kwenye biashara ya mpira. Kosa kubwa ambalo wengi hulifanya ni kutoamini mpira ni biashara.

Na kuacha kuutazama mpira katika jicho la kibiashara. Wengi wanaona mpira ni kujitolea tu, yani wachezaji wajitolee hata kama wakiwa na njaa.

Mashabiki wajitolee pesa zao mfukoni kuichangia timu. Hiki kitu hatuwezi kukiishi leo. Yani hapa Yanga wanajaribu kuishi jana kwenye nuru ya leo.

Kwa kifupi wako gizani, hawaendi na muda kabisa ndiyo maana timu yao inaendeshwa kwa kudra za mwenyezi MUNGU.

Ndiyo maana wachezaji wanagoma kwa sababu hawajalipwa haki yao ƴa msingi (mshahara) hapo unaambiwa hii timu inagombania kuwa bingwa wa ligi kuu Tanzania bara.

Huwezi kuwa na kikosi chenye njaa ya tumbo ukapata ubingwa. Hapa tutajidanganya mchana kweupe kabisa. Lazima tuitoe njaa.

Tupate pesa ambazo tutawalipa wachezaji. Wachezaji wapate moyo wa kupigana vizuri uwanjani ili wabakize kombe.

Tunapataje hizo pesa ? Hawa hawa mashabiki ambao kila tukienda mkoani wanatupokea kwa furaha.

Hawa mashabiki wanaojitolea kwenye kila hali ndiyo wana pesa zetu. Yajengwe mazingira mazuri ya kuwashawishi watoe pesa zao mfuƙoni kwa wingi.

Tuwatumie vizuri hawa mashabiki wengi ambao tulionao ili kuondokana na hii fedheha, tusipowatumia vizuri hawa mashabiki kuna siku MUNGU atawatoa Yanga na kuwapeleka kwenye timu nyingine ambayo inajua kutumia mtaji wa mashabiki.

Sambaza....