- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
Saa sita mchana ndiyo muda ambao nilianza safari kuelekea Temeke, wilaya ambayo imebeba uwanja mkubwa hapa Afrika Mashariki na kati.
Uwanja ambao muda huu unatumika kuandaa michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon Under 17).
Uwanja ambao jana ulitakiwa ubebe mechi mbili za kundi A la michuano hii. Kundi ambalo sisi Watanzania tupo.
Na mechi ya kwanza ilikuwa kati ya Angola na Nigeria. Mechi ambayo ilikuwa na mafundisho makubwa sana ndani na nje ya uwanja.
Kikubwa ambacho kilinipa nguvu ya kuchukua karatasi yangu na cha kuandikia ili niandike hii makala. Kuna kitu kikubwa ambacho nilijifunza nje ya uwanja.
Kitu chenyewe ni mashabiki. Hiki ndicho kitu kikubwa sana ambacho nilijifunza Jana. Kwanini ?. Wakati nafika kwenye uwanja mkuu wa Taifa nilikuta mashabiki wapo uwanjani.
Hawakuwa wengi wa kutisha lakini walikuwepo wa kiasi chake tofauti na wengi ambavyo walivyokuwa wamefikiria awali.
Mechi hii ya Nigeria na Angola ilikuwa inachezwa muda mmoja na mechi ambazo zilikuwa zinawahusisha watu ambao wana hatimiliki ya mpira wa miguu hapa Tanzania.
Watu ambao wameigawana Tanzania katikati. Upande mmoja kuna rangi ya njano na kijani na upande mwingine kuna rangi nyekundu na nyeupe.
Hawa ni Simba na Yanga. Kwa matarajio ya wengi muda huu ilitazamiwa watu wote wangekuwa kwenye luninga zao wamewasha huku wakiangalia mechi hizi.
Lakini ilikuwa tofauti kabisa, sawa wengi walikuwepo luningani lakini kuna wengine walikuwepo kwenye uwanja wa Taifa kutazama mechi kati ya Nigeria na Angola.
Hapa ndipo nilipotulia kidogo. Kitu cha kwanza ambacho kilikuja akilini mwangu ni kuwa Watanzania wanapenda sana mpira.
Nilitulia, sikutaka kujipa hitimisho hapo hapo. Nilikaa zangu kutazama vipaji vikubwa vya vijana wa Nigeria. Vipaji ambavyo kwa miaka mitatu ijayo tutavisikia vipo Ulaya.
Vipaji ambavyo miaka kadhaa ijayo vitakuja na hadithi nyingine. Hadithi ambazo zitakuwa na kibwagizo kimoja tu, huyu aliwahi kuja Tanzania kwenye mashindano ya vijana ya Afcon.
Ndiyo hadithi pekee ambayo tutaisumilia miaka kadhaa ijayo. Tuachane na hiki turudi kwenye kiini cha makala hii.
Baada ya mechi kuisha kulikuja mechi ambayo kimsingi ndiyo ilikuwa inasubiriwa sana kwa kipindi hicho kwa sababu tu timu yetu ilikuwa inacheza.
Mechi ambayo wengi tulikuwa na mategemeo ya kupata ushindi ili tu tuweze kuingia kwenye nafasi ya nusu fainali ya michuano hii.
Mechi ambayo mashabiki wengi sana walikuja, mashabiki ambao walikuwa na uchungu sana na timu yao tena kuzidi uchungu wa wachezaji waliokuwepo uwanjani.
Wachezaji walionekana hawana uchungu na nchi yao kwa kiasi kikubwa lakini mashabiki ambao walikuwa jukwaani walikuwa na uchungu sana.
Kuna wakati walikuwa wanatamani sana kuingia uwanjani. Kuna wakati walikuwa wanatamani kuona mpira ukiingia moja kwa moja golini mwa Uganda lakini ilikuwa tofauti kabisa na matamanio yetu.
Matamanio yetu yalizidiwa na uwezo wetu. Uwezo wetu ulikuwa mdogo sana na matamanio yetu yalikuwa makubwa sana kwa muda huo.
Mwisho wa siku maumivu ndicho kitu pekee ambacho tuliondoka nacho. Mpaka dakika ya 90 mashabiki pale uwanjani walikuwa wanaamini Serengeti Boys wangeweza kusawazisha magoli yote.
Walikuwa na subira, na walikuwa wanawaunga sana mkono hawa watoto lakini mwisho wa siku hakuna kitu ambacho tulifanikiwa kukipata zaidi ya maumivu.
Ndipo hapo tuliamua kurudi majumbani kwetu tukiwa na huzuni iliyochanganyikana na hasira kubwa ndani yetu.
Ushawahi kumuona mtu anahuzuni kubwa huku anatukana ?. Hapana shaka taswira ya mtu huyu alikuwepo ndani yetu kwa kipindi cha Jana.
Tulikuwa tunahuzuni kubwa sana , huzuni ambayo tuliamua kuimalizia kwa kutukana kila aina ya tusi ambalo lilikuja kwenye vinywa vyetu.
Magari ya kubeba abiria stori kubwa ilikuwa kipigo ambacho tulipigwa Jana. Tulilaumu sana, tuliongea sana , tulihuzunika sana mwisho wa siku tukamalizia kwa kutukana tu.
Pamoja na foleni njiani lakini watu hawakuiona. Kitu pekee ambacho walikuwa wanakiongelea kwa uchungu ni hii mechi.
Pamoja na joto la Dar Es Salaam kuwa kubwa lakini hawakuzuia kuonesha wazi wazi hisia zao kutokana na matokeo mabaya ya Serengeti Boys.
Tuacheni utani, Watanzania wanapenda sana timu zao, Watanzania wanapenda sana mpira kupita maelezo.
Mtu alikuwa anaelezea kwa uchungu mpaka kufikia hatua ya kulia kwa sababu ya maumivu tu. Inauma sana, inahuzunika sana.
Hapa ndipo maumivu ya kumpenda mtu ambaye hakupendi yanapokuja. Nahisi ushanielewa vizuri. Hiki ndicho kinachotokea kwa Watanzania.
Wanapenda sana mpira kupita maelezo, lakini hakuna mazingira yoyote ambayo wametengenezewa wao kufurahia kupitia mpira.
Hakuna mfumo bora wa kuzalisha wachezaji bora ambao wangekuwa na uwezo wa kuwafanya wapate matokeo bora ambayo yangeleta furaha kubwa kwao.
Wanaopewa dhamana ya kutengeneza hii mifumo hujisahau kabisa. Na kuna wakati hawapati kabisa muda wa kutazama mahaba makubwa ya Watanzania kuhusiana na mapenzi yao kwenye mpira wa miguu.
Na kinachouma zaidi hawa wanaopenda mpira kupitiliza ni watu masikini. Hawana uwezo mkubwa wa kifedha kwenye mfuko wao.
Uwezo ambao ungewawezesha hata wao kutengeneza angalau kituo kimoja kikubwa chenye wataalamu haswa wa soka la vijana kwa minajili ya kutengeneza wachezaji ambao wangewapa furaha.
Hawana hizo hela , Ila wana mapenzi ya dhati. Na wenye hela hawana mapenzi ya dhati, wana mapenzi ya kununua. Mapenzi ya kujionesha kuwa wanapenda mpira wa miguu.
Ndiyo maana hujitokeza kipindi ambacho timu iko kwenye michuano na kuanza kutoa ahadi ambazo hazina msaada mkubwa, haya ni mapenzi ya pesa siyo dhati kama walivyo wengine.
Wanasahau msingi mkubwa wa kupata timu imara ni kutengeneza mirija inayozalisha vipaji na siyo kutoa ahadi wakati timu iko kwenye mashindano bila kujali mfumo mbovu wa uzalishaji wa hawa watoto.