Kiungo wa zamani wa Manchester United Paul Scholes ameingia kwenye rekodi ya makocha ambao wamezitumikia timu zao kwa kipindi kifupi zaidi baada ya kutangaza kuachia ngazi kuifundisha timu ya Oldham Athletic toka alipojiunga nayo mwezi uliopita.
Scholes mwenye umri wa miaka 44 ameikacha timu hiyo baada ya kuiongoza katika michezo saba, akishinda mchezo mmoja pekee na kufungwa michezo mitatu na kutoka sare michezo mitatu na amesema kuwa anasikitika kuiacha timu hiyo ikiwa bado kwenye nafasi mbaya.
Mchezo wa mwisho wa Scholes kuiongoza timu hiyo ulikuwa ni ule wa jumanne ambapo walicheza na vinara wa ligi daraja la pili Lincoln City na kupoteza kwa mabao 2-0, kabla ya kuandika jana ujumbe mrefu kwa njia ya WhatsApp kuelekea kwa viongozi wa timu hiyo akielezea adhima yake.
“Nasikitika kuwaeleza kuwa nimeshindwa kufanya kama vile nilivyotadhamia kufanya kwenye klabu hii, kwa moyo mkunjufu naomba kuhitimisha safari ya miezi 18 ambayo nilitamia kuwepo hapa katika klabu ambayo nimekuwa nikiiunga mkono kwa muda mrefu, nawatakia wachezaji, viongozi na mashabiki maisha mema,” amesema.
Tayari klabu hiyo imethibitisha kuhitimisha safari ya pamoja na kiungo huyo wa zamani wa Manchester United ambaye kipindi akiwa uwanjani alikuwa akiwakonga nyoyo mashabiki wa United na timu nyingine.
“Klabu ya Oldham inathibitisha kwamba Paul Scholes ameondoka katika majukumu yake, tunashukuru kwa jitihada zake za kuifanya kuwa timu kubwa, tunamtakia mafanikio kwenye maisha yake ya baadae, kuhusu kocha atakayeshika nafasi yake, klabu itamtangaza mapema,” taarifa ya klabu imesema.
Kwa kuondoka klabu hapo Scholes anakuwa miongoni mwa makocha waliowahi kukaa kwa muda mdogo zaidi kwenye vilabu vyao, chini ni orodha ya makocha hao, klabu walizokaa na kipindi walichokaa kabla ya kuachia ngazi.
- Brian Clough, Leeds United- Siku 44 , Michezo nane – 20 Jul hadi 13 Sept 1974
- Les Reed, Charlton – Siku 41, Michezo nane – 14 Nov hadi 23 Dec 2006
- Alex McLeish, Nottingham Forest – Siku 40, Michezo saba – 27 Dec 2012 hadi 5 Feb 2013
- Steve Coppell, Manchester City – siku 33, Michezo sita – 6 Oct hadi 8 Nov 1996
- Paul Scholes, Oldham Athletic – Siku 31, michezo saba – 11 Feb hadi 14 Mar 2019
- Paul Hart, QPR – siku 28, michezo mitano 17 Dec 2009 hadi15 Jan 2010
- Micky Adams, Swansea – siku 13, michezo mitatu – 9 Oct hadi 22 Oct 1997.