Sambaza....

Mlinda mlango raia wa Ujerumani Loris Karius ameandikia barua ya kuomba msaada kwa kupeleka malalamiko kwenye shirikisho la kandanda Ulimwenguni (FIFA) baada ya kukaa kwa kipindi cha miezi minne bila kulipwa mshahara na klabu yake ya Besiktas ya Uturuki.

Jarida la Goal limeandika habari hiyo na kusema kuwa Karius ambaye anacheza kwenye klabu hiyo kwa mkopo akitokea Liverpool ya England amepanga pia kufungua mashtaka ili aweze kulipwa mshahara wake.

Taarifa zimesema kwamba Karius anaidai Besiktas mshahara wa miezi minne wenye thamani ya zaidi ya Bilioni Mbili na tayari imeripotiwa kuwa mawasiliano yake ya kwanza na FIFA yalifanyika Februari 20 ambapo aliandika barua ya malalamiko yake.

Baada ya hapo FIFA wakaiandika barua Besiktas wakiwapa hadi siku 10 kuweza kumlipa mishahara yake mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25 lakini hawakuijibu barua hiyo jambo ambalo linawafanya FIFA kufikiria kuchukua hatua nyingine kubwa zaidi ikiwemo kuiwekea vikwazo klabu hiyo kama ikifahamika imevunja kanuni za FIFA.

Kama itafahamika kuwa wameshindwa kumlipa mshahara mlinda mlango huyo basi Besiktas inaweza kupokonywa alama ama kuondolewa kwenye michuano ya Uropa Ligi, wakati ambapo kwa sasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Uturuki.

Sambaza....