Kati ya mikataba ya ajabu iliyowahi kutokea kwenye mchezo wa soka basi ni huu mkataba wa makubaliano ya awali kati ya shirikisho la soka nchini Morocco na shirikisho la soka nchini Argentina kuelekea katika mchezo wa kirafiki.
Katika mkataba huo Nahodha wa Argentina Lionel Messi amewekewa kinga kubwa ikiwemo baadhi ya vipengele kuwafunga kabisa waandishi wa habari, mashabiki, na hata wachezaji wa Morocco kumkaribia nyota huyo wa soka.
Kwa mujibu wa gazeti la Morocco Al Akhbar ni kwamba moja ya vipengele ni kutoruhusiwa kabisa kumpiga picha Lionel Messi kabla na baada ya mchezo huo, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa Morocco kutotakiwa kabisa kupiga Selfie na Messi.
Mojawapo ya kipengele kingine ni kuvizuia kabisa vyombo vya habari kufanya mahojiano na mchezaji huo iwe kabla hata baada ya mchezo huo, lakini hayo sio mambo ya kushangaza sana kama vipengele vingine.
Jambo lingine ambalo pengine linashangaza zaidi, ni kwa wachezaji wote wa Morocco hawatakiwi kuwa na mchezo wa nguvu kupita kiasi wanapokabiliana na Messi, kwa maana kwamba wanatakiwa kutomchezea rafu kabisa gwiji huyo wa soka, hivyo Messi atacheza kama yupo pekee uwanjani.
Aidha miongoni mwa vipengele vingine kwenye mkataba huo wa awali ni pamoja na shirikisho la soka la Morocco kuhusika na gharama zote katika safari zote za msafara wa Argentina ikiwa ni pamoja na kuwaleta nchini wakitokea Uhispania ambapo watacheza mchezo mwingine wa kirafiki kwenye uwanja wa Wanda Metropolitano dhidi ya Venezuela.
Mbali na hayo pia wameweka masharti ya sehemu ambayo Messi atalala kuwekwa siri kwa siku zote ambazo timu hiyo itakuwa nchini Morocco, pamoja na kumuahikikishia usalama mchezaji huyo pamoja na msafara mzima wa timu ya Taifa ya Morocco.
Morocco wanatarajiwa kuwakaribisha Argentina katika mchezo wa kirafiki uliopangwa kufanyika March 26 kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah uliopo mjini Rabat.