Tangu Mbao FC wapande ligi kuu ya Tanzania bara, Yanga hakuwahi kuibuka na ushindi kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Pamoja na kwamba Yanga hawakuwahi kuibuka na ushindi kwenye uwanja huu, pia walikuwa hawajawahi hata kufunga goli moja.
Makambo amekuwa mchezaji wa Kwanza kutoka Yanga kuifunga Mbao Fc katika uwanja wa CCM Kirumba.
Pia Mwinyi Zahera amekuwa kocha wa kwanza kutoka Yanga kuibuka na ushindi katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya Mbao FC.
Katika mechi hiyo Mbao FC walikuwa wa kwanza kufunga goli dakika chache kabla ya mchezo kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuingia kwa kulisakama lango la Mbao FC na wakafanikiwa kupata goli kupitia kwa Makambo aliyeunganisha mpira wa kichwa kutoka kwa Papy kabamba Tshishimbi.
Kelvin Yondan alipanda kushambulia na krosi yake ilisababisha penalti ambayo Amis Tambwe aliifunga na kuifanya Yanga kumaliza mchezo wakiwa na ushindi wa magoli 2-1.
Kipi kimeisaidia Yanga?, katika mechi dhidi ya Simba nilisema kitu kimoja. Yanga waliwapanga kina Makambo na Amis Tambwe kwa pamoja.
Lakini washambuliaji hawa walinyimwa watu wa kupiga krosi baada ya asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga kusimama katikati ya uwanja.
Leo hii Yanga walikuwa wanatumia krosi nyingi kuwafikia kina Makambo, hali ambayo ilisababisha Yanga kupata ushindi.