Sambaza....

Kamati ya maandalizi ya Kandanda Day 2017, tamasha la mpira wa miguu linalofanyika kila mwaka mwezi wa kumi, limekabidhi zawadi ya jezi kwa klabu ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 13 ya Bombom FC.

Bombom FC waliibuka mabingwa katika mchezo wao uliofanyika tarehe 22/10/2017 katika viwanja vya chuo kikuu cha DUCE baada ya kuifunga House of Blue Hope Football Academy kwa mikwaju ya penati.

“Vituo vyote vilikuwa na uhitaji wa vifaa vingi vinavyohusu mpira wa miguu na malezi kwa ujumla, kamati imekabidhi kwa mshindi kwanza kama tulivyoahidi jezi kwa U13 kwa Bombom FC, lakini tunawapongeza pia House of Blue Hope kwa kushiriki nasi”  amenukuliwa Mratibu wa Kandanda Day 2017,  Ndugu Laurian Wajimila.

Kupitia kwa Kocha na Msimamizi Mkuu wa kituo hicho cha kulea vijana cha Bombom Sc na msaidizi wake Katibu wa kituo hicho Ndugu Uwesu Ahmad wameishukuru kamati Kandanda Day  2017 kwa kutimiza ahadi yao. “Licha ya kwamba tuna changamoto nyingi sana, Tunashukuru sana Kandanda Day pamoja na Kandanda.co.tz kwa zawadi hii ya jezi seti 16, ambazo zitasaidia vijana wetu katika michuano mbalimbali” Alisema msimamizi wa kituo hicho Bwana  Hamidu Kibonge.

Kandadna Day 2017
Mratibu wa Kandanda Day 2017, Ndugu Laurian Wajimila akimkabidhi jezi Msimamizi na Kocha mkuu wa Bombom FC, Hamidu Kibonge.
Msimamizi wa tovuti ya Kandanda, Thomas Mselemu akikabidhi mzigo mzima wa jezi baada ya mratibu kukabidhi rasmi

Kwa upande wa Msimamizi wa tovuti ya kandanda.co.tz,  Ndugu Thomas Mselemu, amesema Kandanda Day inatarajiwa kufanyika pia mwakani katika tarehe itakayotangazwa na kamati. “Ni matumaini yetu Bombom FC tutakuwa nao pia na kama tukipata wadhamini zaidi bila shaka washiriki watapata vifaa vitakavyowasaidia zaidi” ameongeza.

Hii ni mara ya tatu Kandanda Day inapeleka zawadi kwa jamii. Mwaka 2015 kituo cha House of Blue hope kilipata msaada wa Vitabu katokana na kampeni ya #MpiraMmojaKitabuKimoja na mwaka 2016 Shule ya msingi Ubungo ilipata madawati 20 kutokana na kampeni ya #MpiraNaDawati.

Sambaza....