Klabu ya soka ya Simba imethibitisha kupitia mtandao wake wa Twitter kuwa ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na klabu ya Pharco ya nchini Misri kuhusu uhamisho wa winga Shiza Kichuya kwenda kujiunga na timu hiyo.
Simba imesema kwamba taarifa zaidi itatolewa baadae baada ya taratibu zote kukamilika, kwa kiungo huyo ambaye alijiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar mwaka 2016.
Kichuya atakumbukwa zaidi kwa kuwa msumbufu hasa Simba ilipokuwa ikikutana na Yanga, zaidi bao lake la kona ya moja kwa moja alilofunga October Mosi mwaka 2016 katika dakika ya 86 kufanya matokeo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Ana amekuwa na misimu miwili ya mwanzo alipojiunga na timu hiyo, na msimu wake wa pili akiwa na Simba aliweza kutengeneza Pasi za mwisho zaidi ya 10 katika michezo ya ligi iliyoisaidia Simba kutwaa Ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.
Mbali na Taji hilo la Ligi Kuu pia mchango wa Kichuya ulionekana alipoisaidia Simba kuchukua Ubingwa wa Azam Sports Federations alipofunga bao muhimu la penati dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma mwaka 2017.
Hata hivyo msimu huu amekuwa sio chaguo la kocha Patrick Aussems, na anaweza kujiunga na timu ya Pharco iliyoanzishwa mwaka 2010 na inayoshiriki ligi daraja la daraja la pili nchini Misri.