Klabu ya soka ya Simba imefanya mazoezi yake ya mwisho leo katika uwanja wa Bokko Beach kabla ya jioni kuelekea Misri katika jiji la Alexandria katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Africa dhidi ya vinara wa kundi Al-Ahly.
Tovuti yako ya kandanda.co.tz ilipata wasaa kidogo wa kuzungumza na mshambuliaji wa Simba sc na timu ya Taifa (U-23) Adam Salamba ambae pia ni mchezaji wa zamani wa Standa United ya Shinyanga na Lipuli fc ya Iringa.
Katika siku za hivi karibuni nyota huyo wa Simba ameonekana ni mwenye kujituma sana akiwa mazoezini huku pia akifanya mazoezi binafsi ya pumzi na ya viungo bila kusimamiwa na mtu. Ndipo tovuti ya kandanda ilipovutiwa na juhudi zake ikataka kufahamu ni kipi kimepelekea kubadilika hivyo.
Adam Salamba “Ili uwe mchezaji nyota ni lazima ufanye mazoezi yako binafsi na ya ziada tofauti na yale anayokupa mwalimu. Mazoezi yanaumiza na ni lazima uumie ndipo uwe nyota katika timu.
Adam Salamba ndie mshambuliaji mwenye umri mdogo kabisa katika safu ya ushambuliaji ya Simba iliyo chini ya wazoefu kama kina John Bocco Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambapo alikiri kuongeza vitu vya kujifunza anapokua na wazoefu hao.
Salamba pia ameongeza “Mpira sio maneno mpira ni vitendo hivyo kwa hiki ninachokifanya kitaonekana uwanjani. Sipendi kuongea sana ili vitu vitajibu uwanjani. Hata wakati nilipokua Lipuli ni hivi ndivyo nilikua nafanya, mazoezi binafsi ndio yamenifikisha hapa nilipo.
Adam Salamba ni miongoniwa nyota 20 waliochaguliwa kueleka Misri huku leo jioni timu ikitarajiwa kuondoka.