Sambaza....

Kocha Mkuu wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amepanga kesho Jumanne Desemba 5, 2017 kuanza kufanyia kazi upungufu ulioonekana kwenye mchezo dhidi ya Libya  uliofanyika Jumapili Desemba 3, mwaka huu.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kenyatta ulioko Machakos hapa nchini Kenya, Tanzania Bara ilipata sare katika safari ya kuwania Kombe la Cecafa – michuano inayofanyika hapa Kenya.

Ninje amesema katika mchezo huo wa kwanza waliecheza katika kiwango cha kuridhisha na kikubwa anataka kuangalia namna ya kufanyia kazi upungufu ikiwa ni pamoja na pale timu inapopoteza mpira.

Anasema kwenye mchezo dhidi ya Libya timu ilicheza kuanzia nyuma kupitia sehemu ya kiungo na kuunganisha sehemu ya ushambuliaji – jambo ambalo limemfurahisha kwa namna timu ilivyotengeneza nafasi.

Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar Heroes, Ninje amesema ni mchezo mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili zinapokutana.

“Lakini kuanzia mazoezi ya kesho nitaiandaa timu kupata ushindi na nimepanga kwenda kuitazama Zanzibar itakapocheza mchezo wake wa kesho dhidi ya Rwanda,” amesema.

Amesema ataiangalia Zanzibar Heroes kiufundi ili kubaini upungufu wao ili naye ajue namna atakavyoweza kutumia nafasi hizo kwenye mchezo unaofuata.

“Ni fahari kwa timu zetu hizi mbili kila mmoja kupambana kupata pointi bahati nzuri wao wanacheza kesho kwa hiyo mchezo wao nitautumia kutazama mapungufu (upungufu wao) yao yatakayoweza kutusaidia,’’ alisema Ninje.

Leo Desemba 4, mwaka huu asubuhi kikosi cha Kilimanjaro Stars kimefanya mazoezi ya kuondoa uchovu baada ya mechi ya jana kabla ya hapo kesho kuanza rasmi kujiandaa kwa mchezo huo unaofuata.

Mbarak Yusuph ndiye mchezaji pekee ambaye hakufanya mazoezi hayo baada ya kuumia misuli kwenye mchezo wa jana dhidi ya Libya.

Mbarak atapumzishwa kwenye mchezo unaofuata ili kuwa tayari kuikabili Rwanda.

Leo jioni Kocha Ninje atakutana na wachezaji kuutathmini mchezo wa Libya ambao ulimalizika kwa sare ya bila kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.

Kilimanjaro Stars ipo kundi A pamoja na timu za Zanzibar, Libya, Rwanda na wenyeji Kenya.

Kenya wana pointi tatu baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 wakati Kilimanjaro Stars na Libya wana pointi 1 kila mmoja baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo wao wa kwanza wakati Zanzibar na Rwanda wenyewe hawana pointi huku Zanzibar ikiwa haijashuka dimbani katika kundi hilo.

Sambaza....