Kuelekea mchezo wa kwanza wa makundi ya klabu bingwa Africa klabu ya Simba inapata pigo katika safu yake ya ulinzi baada ya kiraka wake Erasto Edward Nyoni kuumia katika michuano ya Mapinduzi huko Zanzibar na kumfanya kuukosa mchezo huo wa kwanza utakaopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Erasto Nyoni amekua mchezaji muhimu katika michezo ya awali ya kuwania kwenda hatua ya makundi huku akicheza michezo yote minne ya awali akiwa na “partner” wake Pascal Wawa. Kwa kiasi kikubwa uwepo wa Nyoni uliifanya ngome ya Simba iwe imara na kufuzu makundi.
Erasto Nyoni aliumia katika mchezo dhidi ya KMKM katika dakika ya 41 ya mchezo baada ya kuchezewa vibaya na nahodha wa KMKM na kupelekea kupata majeraha ya goti na kutolewa na machela nje ya uwanja.
Baada ya Nyoni kupata majeraha wapenzi wengi wa Simba wamekua na hofu juu ya kumkosa mlinzi huyo na kuanza kumlaumu mwalimu Auseems kwa kuchezesha kikosi kamili. Lakini kwenye uhalisia Simba haina pengo kubwa kiasi hicho lililoachwa na Nyoni na hii ni kutokana na kikosi cha Simba kilivyo.
Pengo la Nyoni litakavyozibwa:
1.Juuko Mursheed.
Hakuna mwenye shaka na uwezo wa mlinzi huyu wa timu ya Taifa ya Uganda. Juuko ni ingizo safi na salama ambalo mwalimu Auseems atalitumia kuziba pengo la Nyoni bila shaka yoyote, hii ni kutokana na uzoefu wake haswa kutoka kwenye Afcon akiwa na Uganda pia michezo mingi aliyocheza akiwa na Simba. Moja ya shughuli zake alizofanya ni pamoja na mchezo wa ugenini wa kombe la shirikisho Africa kati ya Simba na Al-Masry.
2.James Kotei
Kiungo huyu kutoka Ghana amekua akifanya kazi kubwa sana katika ukabaji haswa katika eneo la ulinzi wa Simba. Kotei anaweza kua mbadala sahihi wa Nyoni kutokana na uwezo wake pia wa kucheza beki wa kati kwa ufasaha mkubwa, aliweza kutumika hivyo msimu uliopita akiwa chini ya Pierre Lenchentre. Kwa kumpanga Kotei kama beki wa kati na si kiungo maana yake ni kumpa mwalimu nafasi nyingine ya kuwatumia viungo wengine kama Ndemla, Niyonzima ama Mzamiru kucheza eneo la kati na Mkude Jonas.
3. Paul Bukaba
Paul Bukaba amekua akiingia na kutoka katika kikosi cha kwanza cha Simba, hivyo kujiamini kwake na kuaminiwa na mwalimu kunaweza kumfanya akawa chaguo la tatu katika kuziba pengo la Erasto Nyoni.