Sambaza....

Uchaguzi wa Yanga umeshafikia hatua nzuri sana. Hatua ya kampeni. Hatua ambayo viongozi hutumia lugha ya ushawishi kwa wanachama.

Lugha ambayo huamini kabisa inaweza ikawapa nafasi ya kuongoza. Kuongoza ni kazi ngumu sana ambayo wengi huichukulia kwa wepesi.

Wepesi ambao huzalisha ukawaida usio wa kawaida katika mioyo yetu. Ndiyo maana hata wakati wagombea wengi wanapobeba fomu huwa wanafikiria kawaida sana.

Hawajikani nafsi zao, hawajui uzito wa fomu ambazo huzibeba. Kwao wao ule wepesi wa karatasi huona ndiyo wepesi wa kuongoza.

Hakuna maono ambayo huyabeba katika kichwa chao. Akili yao kubwa hufikiria namna ambavyo atajiimarisha yeye na siyo kuimarisha klabu.

Mwisho wa siku baada ya wao kumaliza muda wao huiacha klabu katika mazingira mabovu sana, mazingira ambayo klabu haiwezi kujiendesha.

Yanga ina umri mkubwa sana, miaka zaidi ya 80. Umri wa mzee ambaye anasubiri siku zake za kwenda kuonana na mwenyezi MUNGU.

Umri ambao mzee huyo hana nguvu yeyote ya kupigana tena , ujana ushamkimbia, nguvu zimeshampotea katika mwili wake.

Ndiyo umri ambao Yanga ipo. Ndiyo umri ambao Yanga wanao na hawaoni kabisa aibu ya kuwa kwenye umri huo bila kufanya kitu chochote cha maendeleo.

Yanga bado haijajitegemea mpaka sasa!, bado inaomba omba kwa kupitisha bakuri. Klabu kubwa kama Yanga inaendeshwa kwa bakuri.

Ni kitu kinachouma sana lakini kinaonekana ni kitu cha kawaida sana kwa wengi hasa hasa viongozi. Na hii ni kwa sababu moja tu.

Wakati wanaenda kuchukua fomu waliona ni kitu cha kawaida sana ile fomu, yani waliichukulia kwa ukawaida usiyo wa kawaida ile fomu.

Wakaiona nyepesi sana pale walipoishika mkononi mwao. Kitu kilichowaaminisha kuwa kuongoza ni kitu chepesi sana.

Waliamini kuiongoza Yanga ni sawa na wepesi wa karatasi ya fomu waliochukulia kwa ajili ya kugombea nafasi ya kuiongoza Yanga.

Hata walipoingia madarakani walifanya vitu vya kawaida sana. Na mwisho wa uongozi wao ulipofika Yanga ikabaki kuwa ya kawaida sana.

Ikawa haina nguvu yoyote ile, haina hata uwezo wa kulipa mishahara ya wachezaji. Mchezaji anakaa mpaka miezi minne bila kulipwa mshahara.

Hili ni jambo la kawaida sana kwa viongozi wa Yanga. Kawaida mno, hata haliwaumini. Wataanzaje kuumia wakati wao mshahara wanapata?

Watawezaje kuumia wakati wao ndiyo wanajipangia kujiingizia mshahara kila baada ya mwezi kuisha?

Watawezaje kuumia wakati wanaitumia Yanga kwa manufaa yao binafsi?, wanalitumia neno YANGA kujiingiza pesa mfukoni mwao.

Hakuna anayefikiria namna ambavyo anaweza kuifanya Yanga iwe na mfuko uliotuna. Mfuko ambao ambao una hela nyingi za klabu.

Hela ambazo zinaweza kuzisaidia Yanga hata kulipa mshahara kwa wachezaji wa Yanga. Hela ambazo zitawafanya wachezaji wasifikirie kugoma.

Wafikirie tu kucheza mpira. Mgomo kiwe kitu ambacho hakina nafasi katika akili yao. Yani wachezaji wawe na utulivu wa nafsi na akili yao.

Timu iweze kushindana na vilabu vikubwa bara Afrika. Ni timu kongwe tena timu kubwa hapa nchini. Ilitakiwa iwe na uwezo wa kusajili mchezaji kutoka ligi kuu ya Misri.

Yani mchezaji kutoka ligi kuu ya Misiri atamani kuchezea Yanga. Hiki kitu kilikuwa kinawezekana na lakini kwa sasa hakipo.

Na hii ni kwa sababu moja tu. Viongozi waliopita wa Yanga wameifanya Yanga iwe ya kawaida, Yanga isiyo kuwa na ushindani mkubwa.

Yanga isiyokuwa na uchumi uhuru. Yanga isiyotegemea hata bakuri la mashabiki ili waweze kuiendesha timu yao.

Yanga ilitakiwa kutengenezea bidhaa zenye nembo ya Yanga hawa mashabiki wa Yanga kuliko kuwachangisha kwa kutumia bakuri.

Jezi ya Yanga ilitakiwa kabisa kuwa na nembo nyingi ya wadhamini wengi ambao wangeisaidia Yanga kujiendesha vizuri.

Lakini viongozi hawakuwa na maono ya kuifanya Yanga iwe mbali. Na kuna wakati Yanga ilichagua kiongozi mwenye pesa.

Kwa kuamini kiongozi huyo angetumia pesa zake kwa ajili ya kuiendesha timu. Sawa kuna wakati hakukuwa na njaa Yanga.

Kulikuwa na neema, kulikuwa na furaha lakini ilikuwa furaha ya muda mfupi. Furaha ambayo ilipotea baada ya kiongozi huyo mwenye pesa kuondoka.

Na kuiacha Yanga na umasikini wake , Yanga ambayo haina uwezo wa kulipa mshahara kwa wachezaji, Yanga yenye mateso makubwa sana.

Lakini kwenye hili zoezi la uchaguzi wanatakiwa kabisa kutokesea kama ambavyo walifanya makosa kipindi cha nyuma. Wanatakiwa kuchagua kiongozi mwenye maono.

Kiongozi ambaye ataifanya Yanga iwe klabu kubwa na siyo klabu kongwe kama ambavyo watu wengi wanavyoiita. Yanga yenye uchumi huru na siyo uchumi tegemezi.

Sambaza....