Hawa waliwahi kuwa mhimili wa timu ya Simba, ndiyo hawa ambao walihakikisha timu inafunga na timu inatengeneza nafasi nyingi za magoli. Ndicho kipindi ambacho nilianza kuishuhudia Simba ambayo inawategemea viungo katika suala zima la kufunga.
Hakukuwepo na mshambuliaji wa kati ambaye alikuwa anaibeba Simba kipindi hicho . Washambuliaji wote waliokuwepo katika kikosi cha Simba walikuwa likizo. Ndicho kipindi ambacho Laurent Mavugo alipoamua kuchukua likizo yake ya kutokufunga. Hakutaka tena kufunga sana kama ambavyo alikuwa anafanya alipokuwa ametoka.
Miguu yake ilikuwa mizito sana kuupelekea mpira katika nyavu. Hata kichwa chake hakikuwa na nguvu tena ya kupeleka mpira nyavuni. Simba ikabaki mkiwa hata Juma Luzio naye alikuwa amezira kipindi hicho. Hakutaka kufunga tena. Hakuitaka kazi yake ambayo ilimfanya aje duniani.
Ndiyo ukawa mwanzo wa Simba kuwaachia ubingwa Yanga kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, kwa sababu tu washambuliaji wao wa kati walikuwa wamezira kufunga. Jukumu lao kuu walilisahau sana. Ikabidi Mohammed Ibrahim, Mzamiru Yasin na Shiza Kichuya kuchukua jukumu hili wakishiana na Ibrahim Ajib.
Timu ikawa mgongoni mwa viungo. Timu ikawa inapata magoli mengi kupitia hawa viungo. Hata mfungaji bora wa klabu alikuwa kiungo. Walifanikiwa kujitengenezea upendo mkubwa ndani ya mioyo ya mashabiki kwa sababu tu ya kiwango ambacho walikuwa wanakionesha uwanjani.
Timu ikawa ya Shiza Kichuya, Mzamiru na Mohammed Ibrahim. Hata kipindi ambacho mmoja wao alikosekana timu ilionekana na upweke sana. Hawa ndiyo walionekana kama wachezaji ambao wangekuja kufanya vizuri kwa muda mrefu ndani ya klabu ya Simba na hii in kwa sababu walikuwa wanaishi kisasa.
Dunia ya sasa ya mpira ilikuwa inawahitaji sana wao. Dunia ambayo washambuliaji wakati wanapotea kwa kiasi kikubwa. Dunia ambayo viungo wa kati na wa pembeni ndiyo mhimili mkubwa. Hii ndiyo dunia ambayo Mzamiru Yasin , Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim walikuwa wanaishi. Na ndiyo ilikuwa dunia sahihi kabisa kwao kwa sababu tu walikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi nyingi za magoli.
Kwa hiyo ilikuwa ngumu kwa kocha yeyote kumkataa mchezaji wa aina hii kwa sababu ndiyo aina ya mchezaji ambaye anatakiwa kwenye dunia hii mpya ya mpira.
Mpira wetu uliwatazama kama watu ambao watakuwa na wakati mzuri sana na jezi ya Simba pamoja na maisha ya mpira kwa ujumla. Tumaini lilikuwa kubwa sana kwao, wengi tulikuwa mashabiki wao. Tulitamani kuwaona uwanjani, na kila tulipokuwa tunawaona mioyo yetu ilijawa na furaha kubwa.
Hii ni kwa sababu moja tu , walijua kutufurahisha ndani ya uwanja. Na tulitamani kuwaona wakiendelea kutufurahisha kila muda. Lakini kwa bahati mbaya muda huu wamekuwa hawana nafasi kubwa ndani ya kikosi Simba. Nguvu ya kupigania kipaji chao imepungua.
Nafasi yao ndani ya kikosi cha Simba, hawapati tena muda mwingi wa kucheza kama awali ambavyo walivyokuwa wanaupata. Ushindani ni kitu cha kawaida katika maisha, na siku zote ushindani huja kumwiimarisha mwanadamu yeyote. Hakuna mwanadamu anayeimarika kwa mafanikio.
Changamoto huja kutuimarisha sisi. Changamoto huja kutufanya wakubwa. Changamoto ni kitu bora kama kikichukuliwa katika mtazamo chanya. Najua muda huu hawana nafasi, najua wanachangamoto kubwa sana kwa kipindi hiki, lakini wanatakiwa kuzitumia changamoto na kurudi tena. Binafsi nimeukumbuka utatu wao.
Utatu ambao ulikuwa bora zaidi. Utatu ambao ulikuwa umejaa vipaji kubwa ndani yao. Utatu ambao ulijizolea mashabiki wengi nchini. Naamini bado wana nafasi kuchukua mamba zao ambazo wameziazimisha kwa wengine. Zile namba ni zao kabisa, siku wakitoka usingizi watazichukua na kuendelea kuufanya utatu wao kuwa imara kwa mara nyingine tena.