TIMU ya Taifa ya Vijana ya Tanzania, Serengeti Boys imebeba taji la michuano ya Vijana kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) U17 kwa kuifunga Angola kwa mikwaju ya penati.
Serengeti imechukua ubingwa huo kwenye michezo hiyo maalumu iliyofanyika Botswana kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Angola ambao ni mabingwa wa ukanda wa COSAFA, walianza kupata bao dakika ya 38 kupitia Morais kabla ya Kelvin Pius John ‘Mbappe’ kusawazisha dakika ya 74 na pambano hilo kulazimika kupelekwa kwenye matuta na vijana wa Tanzania wakafanikiwa kubeba ubingwa huo kule Botswana.
Timu ya Taifa ya vijana wa Tanzania walipata nafasi hiyo ya kucheza fainali baada ya kuitoa timu ya vijana ya Zambia kwa mikwaju ya matuta katika nusu fainali, baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja dakika 90.
Serengeti boys pia imefanikiwa kutoa mchezaji bora wa mashindano baada ya nahodha wake anaechezea nafasi ya kiungo kuchaguliwa kama mchezaji bora wa mashindano.
Serengeti boys wametwaa ubingwa huo huku wakiwa wageni waalikwa kutoka katika ukanda wa CECAFA. Pia wakitarajiwa kuwa wenyeji wa fainali za Afcon U-17 zitakazofanyika jijini Dar es Salaam Afrika mwakani.