Kocha wa timu ya Monaco Thierry Henry amesema haoni wa kumlaumu wakati akiwa hajashinda mchezo wowote toka alipokabidhiwa timu hiyo.
Henry amesema kwa sasa wanachoangalia ni mchezo ujao dhidi ya Club Brugge wa ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na kwamba anatamani kuona wachezaji wake wakipambana ili kupata ushindi wakati wakizika yaliyotokea nyuma.
“Mchezo dhidi ya Club Brugge ni mchezo mkubwa kwetu, tunahitaji alama tatu, japokuwa wengine wanasema tulipaswa kuchukua alama hizi tatu katika mchezo uliopita, huwezi kubadilisha kila kitu ndani ya wiki mbili lakini pia hatupaswi kuumiza kichwa kwa ajili ya hilo,” Henry amesema mchezaji wa zamani wa Arsenal na Barcelona na pia kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Ubeligiji.
Mpaka sasa Henry ameiongoza Monaco michezo minne lakini hajapata ushindi katika mchezo wowote jambo ambalo limekuwa likiibua maswali mengi kuhusu uwezo wake wa kukiongoza kikosi hicho.
Katika michezo hiyo minne amepoteza dhidi ya Strasbourg na Reims kabla ya kutoka sare na Dijon katika michezo ya Ligi pamoja na mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa hatua ya makundi ambapo walitoka sare na Club Brugge.
Usiku wa Jumanne kwa mara nyingine Monaco watakuwa kwenye uwanja wa Stade Louis II, mjini Monaco na Henry amesisitiza kuwa yeye pamoja na wachezaji wanatakiwa kujitoa kwa hali na mali ili kuweza kupata alama katika mchezo huo na kuacha visingizio visivyokuwa na maana.
Monaco wapo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi A lenye timu za Borrusia Dortmund, Atletico Madrid na Club Brugge wakiwa na alama 1 katika michezo mitatu, hivyo ni muhimu kushinda katika mchezo wa leo kama wanataka kufufua matumaini ya kusonga mbele.