Kikosi cha timu ya Simba Jumapili kiliwakaribisha Stand United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam na kuwapa chuma tatu kwa bila katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara.
Stand united hii ambayo ilifungwa mabao manne kwa matatu dhidi ya Yanga katika dimba la Taifa, pia mwaka jana iliweza kutoka suluhu ya mabao matatu kwa matatu katika uwanja huohuo.
Katika mchezo huo wa Jumapili Simba iliwakosa wachezaji wake muhimu tena wa kikosi cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo adhabu na majeruhi. Simba iliwakosa Jonas Mkude (majeruhi), John Bocco, James Kotei na Erasto Nyoni (kutokana na adhabu ya kufungiwa).
Lakini kwa jinsi timu ilivyocheza na kupata matokea huwezi kuhisi kua iliwakosa wachezaji muhimu tena wa kikosi cha kwanza ambao wote kwa kiasi kikubwa walifanikisha ubingwa wa klabu yao msimu uliopita.
Pengo la Erasto Nyoni lilizibwa vizuri na Juuko Mursheed na kufanya eneo lá ulinzi kuendelea kua imara huku Said Hamis Ndemla “Daktari” alicheza eneo lá kiungo mkabaji akiziba vizuri nafasi iliyoachwa na kina Jonas Mkude na James Kotei.
Ikumbukwe Ndemla amezoeleka akicheza kama kiungo wa ushambuliaji lakini katika mchezo dhidi ya Stand United alicheza kama kiungo wa ulinzi na kufanya vyema katika nafasi hiyo na kuzidi kumpa mtihani mwalimu Patrick Ausems katika upangaji wa kikosi.
Lakini pia katika eneo la ushambuliaji lilimkosa nahodha John Bocco lakini muunganiko mzuri wa Meddie Kagere na Emmanuel Okwi kuliwafanya walinzi wa Stand United kulala na viatu, hivyo kutokuwepo kwa John Bocco kufanya kama hakijatokea kitu.
Wakati Ligi ilipomalizika na vilabu kuanza kufanya usajili msemaji wa Klabu ya Wekundu wa Msimbazi ndugu Hajji Manara alisema watahakikisha wanafanya usajili utakaowawezesha kushiriki michuano yote bila shida. Akimaanisha michuano ya kimataifa, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la mapinduzi.
Hata baada ya usajili kuisha na timu kwenda kambini Uturuki msemaji huyo bado aliendelea kujigamba kua wana kikosi kipana msimu huu.
Kwa hakika kilichotoe katika mchezo dhidi ya Stand United kimedhihirisha upana wa kikosi cha SimbaSc msimu huu.