MICHEZO mitatu ya ligi kuu Tanzania Bara inataraji kupigwa leo Ijumaa katika miji mitatu tofauti. Ndanda FC ambayo ilikwama mkoani Singida kutokana na hali ngumu ya kiuchumi wiki iliyopita watakuwa nyumbani Nang’wanda Stadium, Mtwara kuwakaribisha Mbeya City FC.
Mwadui FC ambayo imeshinda mara moja tu katika michezo nane iliyopita itakuwa nyumbani Mwadui Complex, Shinyanga kucheza na Ruvu Shooting ya Pwani. Ushindi unaweza kuwaondoa Mwadui mkiani mwa msimamo.
Mabingwa mara moja wa kihistoria, Azam FC itakuwa nyumbani Azam Complex Chamanzi kuwavaa African Lyon. Azam inaongoza ligi ikiwa na alama 18 baada ya kushinda mara tano na kutoa sare michezo mitatu kati ya nane waliyokwishacheza.
Ni mchezo muhimu kwa kila timu. Wenyeji wapo nafasi ya 15 wakiwa na point inane katika michezo tisa waliyocheza. Ndanda wamekuwa na beki dhaifu, hadi kufikia michezo tisa waliyokwishacheza timu hiyo ya Mtwara imeruhusu jumla ya magoli 14.
Pia wamekuwa na safu butu ya mashambulizi. Vitalis Mayanga amefunga magoli manne kati ya sita yaliyofungwa na timu yake katika michezo nane iliyopita. Ni lazima wapandishe umakini wao katika kujilinda ili Ambokile Eliud asiendelee kutikisa nyavu za wapinzani wake msimu huu.
Mshambulizi huyo wa City ( Ambokile amekwishafunga magoli saba msimu huu na kujikita kileleni mwa orodha ya wafungaji. City licha ya kwamba nao si bora sana katika ngome lakini wanaweza kufunga. Timu hiyo ya Mbeya imefunga magoli 12 na kuruhusu 13 katika michezo yao tisa iliyopita hali inayowafanya washike nafasi ya tisa wakiwa na pointi 13 ( alama tano zaidi ya Ndanda)
Shooting ilianza msimu kwa kasi ndogo, ikiwa imecheza michezo nane na kukusanya alama tisa timu hiyo ya Pwani imeshinda michezo miwili, sare tatu na vipigo vitatu itakuwa na kazi kubwa wakati watakapoitembelea Mwadui walio mkiani mwa msimamo na alama zao tano kufuatia ushindi mmoja, sare mbili na vipigo vitano katika michezo nane iliyopita.
Shooting imeruhusu magoli tisa na kufunga itaendelea kumtegemea mshambulizi wake Said Dilunga ambaye tayari amefunga mara mbili msimu huu. Mwadui pia hawana beki nzuri kwani katika michezo nane wameruhusu jumla ya magoli kumi huku safu yao ya mashambulizi ikionekana kuwa butu kufuatia kufunga magoli sita tu. Hii ni mechi nyingine ambayo iinataraji kuwa kali na ngumu Ijumaa.
Timu hizi mblili kwa pamoja zilipanda ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2008/09. Tangu wakati huo, Lyon wameshuka daraja mara tatu huku Azam FC ikishinda taji moja la ligi msimu wa 2013/14. Kabla ya Lyon kushuka daraja msimu mmoja nyuma mechi yao vs Azam FC ilimalizika kwa sare ya kufungana 1-1.
John Bocco wakati huo akiwa Azam FC aliiokoa klabu yake hiyo kupokea kichapo kufuatia kusawazisha dakika ya mwisho kabisa ya mchezo katika game ambayo ilitawaliwa na vurugu kubwa mara baada ya kumalizika kwa mchezo.
Mmiliki wa Lyon, Rahim Zamunda alionekana akijibizana kwa hasira na aliyekuwa mtendaji mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba na chanzo cha malumbano yao hayo ni kitendo cha mwamuzi kutomaliza mchezo licha ya dakika kumalizika wakati huo Lyon wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Leo, timu hizo zinakutana tena na Lyon wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa sababu Azam FC imejizatiti msimu huu na inafukuzia taji la pili. Azam ndiyo timu iliyoruhusu magoli machache zaidi katika ligi hadi sasa ( goli moja), imefunga kumi, imeshinda michezo mitano na imetoa sare tatu ambazo zinawafanya wafikishe alama 18 kilel;eni mwa msimamo.
Lyon imekuwa na matokeo mabnaya, katika michezo yao tisa waliyokwishacheza timu hiyo imepoteza mara tano, imeshinda mara moja na sare tatu. Ipo nafasi ya 18 ikiwa na alama sita tu. Safu yao ya mashambulizi ni butu mno kwani wamefunga magoli matano tu na kuruhusu jumla ya magoli kumi hadi sasa.