Timu ya soka ya Azam ya Jijini Dar es Salaam imeendelea na maandilizi kujiandaa na mchezo wa Ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya African Lyon utakaochezwa siku ya Ijumaa kwenye uwanja wa Azam Complex.
Jaffary Idd Maganga ambaye ni afisa habari wa klabu ya Azam amesema lengo lao kuelekea mchezo huo ni kubakisha alama zote tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani, na hilo linafanyiwa kazi na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Hans Van der Pluijm na Juma Mwambusi.
Amesema hali itakuwa nzuri zaidi pale ambapo wachezaji wao waliopo kwenye majukumu ya timu za Taifa watakaporejea na kuendelea kufanya mazoezi na wenzao kujiandaa na mchezo huo.
“African Lyon ni timu nzuri inayoleta ushindani, lakini sisi tunahitaji kupata ushindi nyumbani, tunasubiri kesho wale ambao wapo kwenye timu ya Taifa, baada ya mchezo wa mwisho na Cape Verde nao watajiunga na wenzao tayari kusubiri mechi hiyo,” Maganga amesema.
Katika hatua nyingine Maganga ametoa taarifa ya hali za Afya za wachezaji Frank Domayo na Paul Peter ambao walikwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi kutokana na majeraha ambao walikuwa wameyapata.
“Domayo tumempokea jana amesharejea na daktari amesema kwamba hatofanyiwa upasuaji, atapata tiba mbadala na atakaa nje miezi miwili bila kucheza, Paul Peter bado yupo Afrika Kusini anasubiri kufanyia upasuaji na atarudi Oktoba 22, lakini pia atakuwa nje miezi miwili kutokana na upasuaji atakaofanyiwa,” Maganga amesema.