Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Barcelona Thierry Henry ametajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaotajwa kurithi kiti cha kocha Leonardo Jardim pindi atakapofukuzwa katika klabu ya Monaco.
Henry mwenye umri wa miaka 41 ambaye alikuwa katika benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Ubeligiji kama kocha Msaidizi kwenye michuano ya kombe la Dunia chini ya Roberto Martnez pia amejumuishwa kwenye orodha ya wanaotajwa kuchukua kibarua katika klabu ya Aston Villa.
Henry alianza kutandaza soka la kulipwa katika Klabu ya Monaco na kuisaidia kushinda taji la Ligue 1 mwaka 1997 na anaweza kurejea tena klabuni hapo kama kocha baada ya matokeo mabaya timu hiyo inayoyapata ikiwa nafasi ya tatu kutoka mwisho wakiwa na alama sita katika michezo tisa ambayo wamecheza hadi sasa.
Taarifa za kidukuzi kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kwamba Jardim ambaye aliwapa ubingwa mwaka 2017 baada ya kusubiri kwa takribani miaka 17 anaweza kufutwa kazi na Henry ni miongoni mwa waliotajwa na kuchukua nafasi hiyo.
Jardim ambaye ni kocha wa zamani wa Sporting Lisbon alichaguliwa kuwa kocha wa Monaco mwaka 2014 na kuibua vipaji vya wachezaji kama Kylian Mbappe, Thomas Lemar, Bernardo Silva na Benjamin Mendy.
Jardim pia aliiongoza Monaco kufika hatua ya nusu fainali ya ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika msimu wa 2016/2017.